Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ameapa kuendelea kuongoza taifa hilo kwa wiki kadha, licha ya shinikizo kutolewa kumtaka aachie madaraka.
Akihutubu moja kwa moja kupitia runinga ya taifa, Bw Mugabe amesema anapanga kuongoza mkutano mkuu wa chama mwezi Desemba.
Maafisa wakuu wa chama hicho cha Zanu-PF walikuwa wameidhinisha hatua ya kumvua uongozi wa chama hicho na kumpatia saa 24 ajiuzulu la sivyo wamuondoe madarakani.
Jeshi lilichukua udhibiti wa serikali wiki iliyopita, huku mzozo kuhusu nani atamrithi ukizidi kutokota. Bw Mugabe ameonekana kupoteza udhibiti wa chama chake.
Mzozo wa sasa ulianza Bw Mugabe alipomfuta kazi makamu wake Emmerson Mnangagwa wiki mbili zilizopita, hatua iliyolikera jeshi ambalo lilitazama hatua hiyo kama jaribio la kumteua mke wake Grace kuwa makamu wa rais na mwisho kuwa mrithi wake.
Mapema Jumapili, Bw Mnangagwa alitawazwa kuwa kiongozi mpya wa chama cha Zanu-PF na mgombea wake wa urais uchaguzi mkuu wa 2018.
Katika mkutano huo pia, Grace Mugabe, 52, alifukuzwa kutoka kwa chama hicho pamoja na maafisa wengine wakuu.
"Mkutano mkuu wa chama (cha Zanu-PF) utafanyika wiki chache zijazo na nitauongoza na kusimamia shughuli zake," Rais Mugabe ameliambia taifa kupitia runinga, akiwa ameandamana na majenerali kadha wakuu jeshini.
Amekiri uokosoaji dhidi yake kutoka kwa Zanu-PF, jeshi na umma, na kusisitiza kwamba ipo haja ya hali ya kawaida kurejea.
"Bila kujali faida au madhara ya jinsi (jeshi) walitekeleza operesheni yao, mimi, kama amiri jeshi mkuu, nakiri kwamba kuna matatizo," amesema, akirejelea hatua ya jeshi ya kuchukua udhibiti wa runinga ya taifa wiki iliyopita.
Hata hivyo, hakuzungumzia uwezekano wake kujiuzulu.
Raia wengi nchini Zimbabwe wameonekana kushangazwa na hotuba ya Bw Mugabe ambaye alitarajiwa na baadhi yao kujiuzulu.
Kiongozi wa chama chenye ushawishi cha maveterani wa vita vya ukombozi wa Zimbabwe Chris Mutsvangwa, ameambia shirika la habari la AFP kwamba sasa Robert Mugabe huenda akaondolewa madarakani baada yake kukosa kujiuzulu leo.
Amesema hotuba ya kiongozi huyo haijazingatia uhalisia.
"Tutafuata njia ya kumuondoa madarakani na tunawataka watu warejee tena barabarani kuandamana."
Maveterani walikuwa wakati mmoja wafuasi sufu wa Bw Mugabe.
Waliongoza uvamizi wa mashamba yaliyomilikiwa na Wazungu mwaka 2000 na wametuhumiwa kwa kutumia ghasia na fujo uchaguzini kumsaidia Mugabe kusalia madarakani.
Lakini mwaka jana, waliacha kumuunga mkono.
Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai ambaye wakati mmoja alihudumu kama waziri mkuu katika serikali ya umoja wa taifa na Rais Robert Mugabe ameambia shirika la habari la Reuters kwamba ameshangazwa sana na hotuba ya Mugabe.
Sawa na baadhi ya raia wengine Zimbabwe, kiongozi huyo wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) amesema alikuwa anamtarajia Mugabe, 93, ajiuzulu baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa serikali wiki iliyopita.
"Nimeshangaa sana. Si mimi pekee, bali taifa lote. Anacheza mchezo fulani. Amevunja matarajio ya taifa lote."
Bado haijabainika ni vipi Rais Robert Mugabe anaweza kuongoza mkutano huo mkuu wa chama cha Zanu-PF mwezi ujao, baada yake kuvuliwa uongozi.
Nyadhifa kwenye chama kuamuliwa kwenye mkutano huo na Bw Emmerson Mnangagwa anaweza kuchukua uongozi wa nchi wakati huo.
Bw Mugabe ameongoza Zimbabwe kwa miaka 37 tangu taifa hilo lilipojipatia uhuru mwaka 1980 kutoka kwa Uingereza.
Hotuba hiyo yake kupitia kwenye runinga Jumapili ilikuwa mara yake ya pili kuonekana hadharani tangu jeshi lilipotangaza kuchukua udhibiti wa taifa hilo katika kile walichosema ni juhudi za kuondoa "wahalifu" ambao wamemzingira rais.
Ijumaa, alihudhuria mahafali katika chuo kikuu wazi cha Zimbabwe, lakini hakutoa tamko lolote wakati huo.
No comments:
Post a Comment