Friday, November 3

Msekwa: Nyalandu halazimiki kuandika barua bungeni


Dar es Salaam. Spika wa zamani, Pius Msekwa amesema Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu hakuwa analazimika kuandika barua kwa Spika wa Bunge wala CCM kwani kuonyesha kwake nia ya kujiunga na Chadema kulitosha kuthibitisha hilo.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, Msekwa ambaye ni makamu mwenyekiti wa CCM mstaafu, alisema kilichomwondoa Nyalandu CCM ni kifungu cha 13 (f) cha Katiba ya CCM kinachoeleza kuwa mtu aliyejiunga na chama kingine chochote cha siasa anapoteza sifa ya kuwa mwana CCM.
“Kilichomwondoa Nyalandu ni kujiunga na chama kingine kinyume na kifungu cha 13 (f). Kuandika barua ni utaratibu tu wa kutoa taarifa kwa chama au Bunge ili wajue,” alisema Msekwa.
Alisema mbali na katiba ya CCM, hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema mtu aliyejivua uanachama wa chama cha siasa anapoteza sifa ya kuwa mbunge.
“Kuandika barua ni utaratibu tu... Chama pia kinaweza kumwandikia Spika ili ajue kwamba yule siyo mwanachama wake,” alisema.
Mbali na mazungumzo ya simu, baadaye Msekwa alituma ujumbe wa maandishi (sms) kupitia simu yake ya mkononi akisisitiza suala hilo.
“Nathibitisha tu maneno niliyoyasema kwenye simu kuhusu Nyalandu na mambo yake. Ni kwamba Nyalandu amepoteza uanachama wake wa CCM kutokana na ibara ya 13(1)(f) ya Katiba ya CCM. Na amepoteza ubunge wake kutokana na Ibara ya 71(1)(f) ya Katiba ya nchi. Hakuna haja ya yeye kuandika barua kwa chama au kwa Spika.
Aliongeza: “Kwa mfano, wakati mimi nikiwa Spika, Mhe. (Augustino) Mrema alikuwa Mbunge wa Temeke kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi. Halafu akaamua ghafla kuhamia TLP. Hakuna barua niliyoandikiwa kuhusu jambo hilo. Lakini tamko lake lilitosha kuniwezesha kuiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba nafasi ya Mrema bungeni ilikuwa wazi kwa hiyo Tume ikachukua hatua za kuijaza. Hakuna utata wowote kuhusu Nyalandu,” alisema Msekwa.
Utata wa barua
Msekwa ametoa ufafanuzi huo wakati kukiwa na sintofahamu kuhusu barua ya Nyalandu kama imepokewa na Ofisi ya Bunge au la.
Wakati Ofisi ya Spika ikisema haijapokea barua hiyo, Nyalandu ameibuka na kuonyesha barua aliyoituma katika mhimili huo.
Nyalandu alimwandikia Spika Ndugai barua hiyo ambayo Mwananchi limeiona Oktoba 30, siku ambayo alitangaza kujiuzulu nafasi zote ndani ya chama hicho ukiwamo ubunge.
Lakini juzi, Ofisi ya Bunge katika taarifa yake ilisema haijapokea barua hiyo badala yake imepokea ile ya CCM Oktoba 30 ikieleza kuwa Nyalandu amepoteza sifa ya kuwa mwanachama wake.
Siku hiyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alihojiwa na Azam TV na kusema kuwa alikuwa hajapokea barua ya Nyalandu lakini hakusema kama alikuwa amepokea ile ya CCM. Alisema endapo angeipata (Barua ya Nyalandu) na kuthibitisha kujiuzulu kwake, angeshauriana na wasaidizi wake kabla ya kuchukua uamuzi.
Ikinukuu barua ya CCM, Taarifa ya Bunge inasema kuwa chama hicho kimekuwa kikifuatilia vitendo na kauli za Nyalandu zisizoridhisha kinyume cha misingi, falsafa na itikadi ya CCM.
“Hivyo, Chama cha Mapinduzi kuanzia tarehe ya barua yao kimemjulisha Mheshimiwa Spika kuwa Lazaro Nyalandu amepoteza sifa za uanachama wa Chama cha Mapinduzi na hivyo kupoteza nafasi zote za uongozi wa ndani wa chama hicho na ubunge kwa mujibu wa ibara ya 13 ya chama hicho,” inasema taarifa hiyo ya Bunge.
Taarifa hiyo inasema kutokana na barua hiyo, Nyalandu amekoma kuwa mbunge na hatua stahiki za kuiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi zinaendelea kuchukuliwa.
Hata hivyo, mara baada ya mbunge huyo kutangaza kujiuzulu, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alikaririwa akisema Nyalandu ametumia haki yake ya kikatiba inayompa haki kila Mtanzania kuwa mwanachama wa chama chochote.
“Ibara ya 20 ya Katiba ya Jamhuri inaeleza kuwa kila Mtanzania ana haki ya kuwa na chama. Ninachoweza kusema ni kwamba kuna jambo la kawaida kabisa lililotokea na wala siyo kubwa kama linavyodhaniwa.”
Polepole alisema wameondoka wazito kwenye chama na kimebaki kimoja na kwamba Nyalandu si sehemu ya wazito, bali ni mwananchi wa kawaida mwenye haki na si mara ya kwanza jambo hili kutokea.
Barua ya Nyalandu
Katika barua yake kwa Spika Ndugai ambayo Mwananchi imeiona pamoja na mambo mengine, alimjulisha kuwa kama alivyotangaza kupitia mkutano wake wa wananabari ameamua kujiuzulu nafasi yake ya ubunge wa jimbo Singida Kaskazini kupitia CCM.
Mwanasiasa huyo anasema licha ya kuondoka CCM na bungeni, bado anaamini kwamba Tanzania inahitaji kupata Katiba Mpya itakayoweka bayana ukomo wa mamlaka ya mihimili ya utawala (Bunge, Serikali na Mahakama) ili kuondoa mwingiliano unaonekana kufanyika kwa wazi sasa.
“Kwa sasa dola haionekani kuwa na mipaka katika dhana ya uongozi wa nchi na hivyo kufanya uwakilishi wetu wa wananchi bungeni kuwa legevu kuliko ilivyokusudiwa kikatiba.”
Nyalandu anawashukuru wabunge wenzake, Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni Freeman Mbowe, maspika wastaafu, Pius Msekwa, Samuel Sitta na Anne Makinda pamoja na Ndugai kwa ushirikiano waliomuonyesha katika vipindi vinne alivyokuwapo bungeni hapo ambako “Alifanya kazi kwa mapenzi makubwa, dhamira ya dhati na moyo mkunjufu.”
Katika barua yake hiyo, Nyalandu anadai kwamba dola imeingilia kwa kiasi kikubwa mfumo wa utendaji na uendeshaji wa CCM hadi kukosa uelekeo, jambo ambalo alisema linawaondolea au kuwapunguzia wabunge wake uwezo wa kufanya uamuzi binafsi wakati wa mijadala au katika kupiga kura kwa kadri ya dhamira zao zinavyowaongoza kama ilivyokuwa wakati wa mchakato wa Katiba Mpya.

No comments:

Post a Comment