Tuesday, November 7

MOI:WAGONJWA KULALA CHINI IMEBAKI HISTORIA


Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) imekuwa na uwezo wa vitanda 340 ya kulaza wagonjwa na kuachana na kulaza wagonjwa chini ya sakafu iliyokuwa inatokana na ukosefu wa vitanda katika taasisi hiyo.

Uwezo wa MOI kuwa na vitanda hivyo imetokana na jitihada za Rais Dk. John Pombe Magufuli kutoa maelekezo ya kutaka watanzania wasipate huduma katika taasisi hiyo wakiwa wamelazwa chini ya sakafu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano wa MOI, Jumaa Almas, amesema kuwa suala la wagonjwa wanaofika katika taasisi ya MOI kulazwa chini ya sakafu limebaki kuwa historia.

Jumaa amesema kuwa Rais Dk.John Pombe Magufuli alichukua jitihada na kununua vitanda ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika hospitali hiyo.

Meneja huyo amesema taasisi ya MOI mazingira ya kutolea huduma katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Dk. Pombe Magufuli, yameboreshwa na kuanza kutumika kwa mradi wa awamu ya tatu ya kupeleka mazingira ya kazi ya kuwa rafiki kwa watoa huduma na wagonjwa.

Jumaa amesema mazingira katika kipindi cha nyuma yalikuwa hatarishi kwa watumishi na wagonjwa kupata maambukizi kutokana na kuwa nafasi finyu ya kuwa na idadi kuliko uwezo wa nafasi.

Amesema awali wodi yenye vitanda 33 ilikuwa inalaza wagonjwa 90 hadi 100 hali ambayo ilikuwa ni wakati mgumu kwa utoaji huduma kwa watumishi kwa nafasi kuwa finyu ambapo idadi ya wagonjwa wa upasuaji imeongezeka hadi kufikia waonjwa 600 hadi 700 kwa mwezi.
Meneja Uhusiano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Jumaa Almas akizungumza na waandishi habari juu ya mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha Rais Dk. John Pombe Magufuli kutoa maelekezo ya kboresha huduma kwa kununua vitanda leo, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment