Akiuliza swali bungeni leo Jumatatu Mnyika amesema Rais John Magufuli akiwa katika ziara Mwanza alitoa kauli ya kibaguzi na kwamba kama si ya kibaguzi basi Serikali itoe kauli ya kuwalipa fidia wakazi hao waliobomolewa nyumba zao.
"Kwa sababu Serikali ilisingizia sheria mimi kama mbunge nilichukua hatua nilileta marekebisho bungeni ili barabara yote iwe mita 60 lakini Serikali ikafanya njama na Katibu wa Bunge aliyeondoka(Thomas Kashililah) kuzuia huo muswada ni lini hasa ikaachana na hizi njama ikakubaliana na Rais na muswada ukaletwa hapa bungeni ili barabara hii iwe na upana wa mita 60? Amehoji.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukizi na Mawasiliano, Elias Kuandikwa amesema sheria mbalimbali za barabara zilipokuwa zikitungwa zilikuwa zikizingatia maendeleo na kwamba Sheria ya Barabara ya Mwaka 1932 ilianisha ukubwa wa barabara katika maeneo yote inapojengwa.
Alimtaka mbunge huyo kuwasiliana na mamlaka za halmashauri za serikali za mitaa ambazo ndio wasimamizi kuona kama kuna mahitaji ya baadhi ya maeneo kufanyiwa marekebisho kwenye sheria hiyo.
"Hakuna njama yoyote na suala la fidia litakwenda kwa mujibu wa sheria," amesema.
Waziri wa Nchi katika ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema Kanuni za Bunge sehemu ya nne inaonyesha jinsi shughuli za Bunge zinavyopangwa na sehemu ya tano inaonyesha namna majadiliano yatakavyofanywa ndani ya Bunge.
"Si kweli kwamba Serikali ilipanga njama na Bunge kuzuia muswada wowote uliokuwa uletwe ndani ya Bunge, suala liloelezwa na Mnyika katika swali la nyongeza si kweli ni suala lililojitokeza katika muswada wake," amesema.
Mhagama amesema Serikali haina utaratibu wowote wa kula njama na Bunge.
Katika swali la msingi Mnyika alitaka kujua ni lini Serikali itawasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya barabara ili eneo la hifadhi ya barabara iwiane na barabara nyingine.
Akijibu swali hilo Kuandikwa amesema Serikali haina mpango wa kufanya marekebisho sheria ili kufanya barabara ya Morogoro kuwiana na barabara kuu nyingine kwa kuwa eneo la hifadhi la barabara hiyo lilotengwa linahitahika kwa ajili ya upanuzi wa barabara ili kuwiana na mahitaji ya sasa na ya miaka ijayo.
No comments:
Post a Comment