Thursday, November 9

Mkuu wa wilaya: Sikuamini kusikia watuhumiwa wa mauaji kituo cha polisi wako huru-4

Mkuu wa Wilaya (DC) Nyamagana mkoani Mwanza,
Mkuu wa Wilaya (DC) Nyamagana mkoani Mwanza, Mary Tesha. 
Mkuu wa Wilaya (DC) Nyamagana mkoani Mwanza, Mary Tesha, amesema hakuamini alipotaarifiwa kuwa askari aliyetuhumiwa kumpiga kinyama na kumsababishia kifo Jackson James Masanja (41), na wenzake wako huru.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni ofisini kwake, Tesha amesema anayafahamu vizuri malalamiko juu ya kifo cha Jackson na tayari ameagiza apatiwe ripoti ya maandishi kuhusu kuachiwa kwa watuhumiwa hao ili achukue hatua.
“Ni kweli wameachiwa, japo sijapata barua lakini hata mimi sikuamini kama kweli wameachiwa ndio maana nimemuagiza OCD (Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Wilaya) aniletee taarifa hiyo kwa maandishi. Kuna polisi kama wawili hivi walikuwa wanatuhumiwa hasa huyo mmoja Obedi ndiye walimtaja sana,” anasema Tesha.
Jackson alikamatwa usiku wa Julai 16 na vijana wa ulinzi shirikishi wa mtaa wa Mkapa, Kata ya Igoma mkoani Mwanza wakiongozwa na mwenyekiti wa mtaa huo, Joseph Tugulu King’eti (57) na baadaye kukabidhiwa kwa polisi akiwa mzima.
Shuhuda anadai wakiwa njiani kuelekea kituo cha polisi, Jackson alikuwa ‘mbishi’ na aliwahoji polisi hao kwa nguvu ni kwanini wamekamatwa na wanawapeleka wapi.
Mwenendo huo unadaiwa kuwaudhi askari waliokuwa kwenye gari hilo kiasi cha mmojawapo kujiapiza kuwa atamfunza adabu watakapofika kituoni.
Walipofika, anasema shuhuda huyo, askari aitwaye Obedi alimshusha Jackson na kuanza kumshambulia kikatili kwa gongo nje ya kituo cha polisi Nyakato kiasi cha askari wengine waliokuwa zamu kumsihi amwachie.
Baada ya kipigo marehemu aliwekwa mapokezi ya kituo hicho na wenzake ambapo alivuja damu nyingi na alifariki alfajiri akipelekwa hospitali kwa matibabu.
Kwa mujibu wa Tesha, mwanasheria wa Serikali mkoani Mwanza alipitia faili la kesi dhidi ya watuhumiwa hao na kuona kuwa hakukuwa na hoja zenye nguvu kuwashawishi kufungua kesi dhidi ya watuhumiwa.
“Mwanasheria anasema huyu marehemu alikuwa handled (alishughulikiwa) na watu wengi katika hatua mbalimbali, kwa hiyo inawezekana kote huko alipokuwa akipita alikuwa anasulubiwa, ndicho alichokuwa ananieleza OCD hapa sasa hivi, so (kwa hiyo) akaona waachiwe ili investigation (uchunguzi) zaidi uendelee ili kujua source (chanzo) cha hicho kifo,” anasema Tesha.
“Sasa nimekuwa nikimfuatilia OCD mara nyingi, huyo uliyemuona anatoka ofisini kwangu ni OCD na ndio nilikuwa namwambia sasa anipatie taarifa ya maandishi, kwa sababu wanasema ni kweli wale watuhumiwa walishtakiwa, walichukuliwa maelezo yao, faili likaenda kwa mwanasheria wa Serikali na ameona hawana kesi ya kujibu.
Mkuu huyo wa wilaya aliamua kulishughulikia suala hilo kwa karibu baada ya kupokea malalamiko toka kwa ndugu wa marehemu na kuitisha mara moja kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ambayo iliamuru watuhumiwa wote wakamatwe baada ya kuridhika kulikuwa na kila dalili za jinai.
Ndugu wa Jackson wanasema mkuu huyo wa wilaya alifanya jitihada nyingi kuwasaidia ikiwamo kutoa Sh 100, 000 ya kununua jeneza na baadaye kumtuma katibu tawala wa wilaya (DAS), Alfred Yohana akamwakilishe katika msiba wa Jackson.
“Nilikaa nao hapa ofisini, actually (kwa kweli) ilibidi niitishe kamati ya ulinzi na usalama kwa sababu niliona hilo jambo ni zito, siwezi kulifanyia maamuzi peke yangu, kwa hiyo tuliwaomba radhi kwa yaliyotokea na tuliwaahidi kwamba haki itatendeka.
“Tuliwapa pesa kidogo ya jeneza na tukawaombea kule hospitali wakapunguziwa gharama za uhifadhi wa mwili kwa sababu hawakujua ndugu yao yuko mochwari, walikuja kujua baadaye sana. Ilikuwa niende mwenyewe hata kwenye kuzika lakini nilishikwa na mambo mengine lakini nikatuma mwakilishi awahakikishie haki itatendeka,” anasema Tesha.
Amesema pindi atakapokabidhiwa ripoti ya maandishi kuhusu sababu za kuachiwa watuhumiwa atakaa tena na kamati yake kwa maamuzi ya mwisho ili kumshauri mkuu wa mkoa nini cha kufanya.
“Nasubiri niletewe ripoti ya OCD kimaandishi kwa sababu mimi kuambiwa kwa mdomo si official (rasmi) ndio maana nimemtaka aniletee kwa maandishi ili mimi na kamati yangu tukae tuone tunamsharuri mkuu wa mkoa achukue hatua gani,” anaeleza.
Aliahidi kuhakikisha haki inatendeka huku akieleza wasiwasi wake kuwa suala hilo lisiposhughulikiwa katika misingi ya haki, linaweza kuwapunguzia wananchi imani kwa serikali yao.
“Kwa sababu kama kweli mauaji yametokea na suala linakuwa handled (linashughulikiwa) kiulaini laini hivi tunaweza kuwafanya wananchi wakose imani hata na Serikali yao.
“Wale (ndugu wa Jackson) wangeona watu wamechukuliwa hatua at least (angalau), inajenga imani kuwa Serikali inalishughulikia, sasa nataka nipate hiyo taarifa tuone tunashauri nini kwa viongozi wa juu, manake ukishaambiwa kitu ni mwanasheria wa Serikali amefanya hilo tena haliko ndani ya uwezo wangu.”
Katibu Tawala: Tuliona suala hili ni zito
Muda mfupi kabla ya kuzungumza na Tesha, Yohana, katibu tawala wa wilaya ya Nyamagana, aliliambia Mwananchi kuwa ndugu wa Jackson kwanza walifika ofisini kwake na Serikali mara moja ilichukua hatua. “Nikawasikiliza nikaona jambo hilo ni serious (zito) na nikaamua kumshirikisha mkubwa wangu, hapo hapo tulichukua hatua, tukaitisha kamati ya ulinzi na usalama, tulijadili malalamiko ikaonekana kwamba lazima yachunguzwe. Mwishoni yalitoka maelekezo kwamba wahusika wakamatwe na uchunguzi ufanyike. Sasa atakayelisemea vizuri ni DC mwenyewe,” alisema Yohana.
RPC aahidi ufafanuzi wa kina
Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC)Mwanza, Ahmed Msangi anakiri kulifahamu vizuri suala ya mauaji ya Jackson lakini anasema hawezi kulizungumzia hadi atakaporudi toka likizo.
“Niko likizo na nitakuwa mtu wa ajabu kuzungumzia suala hilo wakati nipo likizo. Barua ya huyo mama niliiona kwa hiyo subiri nirudi utapata kila kitu. Nimeiona hata ile barua yake aliyoandika kila mahali! Kila mahali. Imeshughulikiwa vizuri tu nikirudi ofisini nitawaeleza ukweli wote,” anasema Msangi.
Wiki moja kabla ya kuzungumza na Msangi, Mwananchi lilikutana na Kaimu RCO, John Rwamlema ambaye alikataa kuzungumzia suala hilo bila kibali cha RPC.Hata hivyo, alikiri kulijua suala hilo: “Mie nalijua hilo suala lakini siwezi kukupa taarifa. Kwani wewe una undugu kwenye familia ile,? Alimuuliza mwandishi.
Akaendelea kuuliza: “Hivi ni mama analalamika au kuna watu wanapika? Unajua mtu anaweza akawa halalamiki lakini watu wengine wanalalamika. “Unajua sisi tuna usemi kwetu kuwa kama kuna msiba ukimuona mtu anakuja analia na wewe utalia tu, na wengine wataanza kulia, huwezi kusema tumwache alie peke yake.
“Ukifuatilia vizuri hicho kilio ni kama cha hivyo. Mimi sikuwepo huko lakini kinachozungumzwa si kama hali ilivyo. Kweli sisi tunajua na kwa kuwa suala hilo ni nyeti na RPC analifuatilia ni vizuri ukaenda wewe kuongea naye,’’ anasema.
Kesho katika sehemu ya tano na ya mwisho ya ripoti hii tutakuletea kilio cha mama wa Jackson, Mary Sebastian (68) katika barua aliyoiandikia Ofisi ya Rais, Ikulu, akiiomba iingilie kati na kuchunguza kifo cha mwanaye ili haki itendeke.

No comments:

Post a Comment