Monday, November 6

MKURUGENZI MKAZI WA SHIRIKA LA MISAADA LA MAREKANI –USAID-AIPONGEZA TASAF.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Misaada la Marekani –USAID- Bwana Andrew Karas amesema shirika hilo litaendelea kuunga mkono kazi inayofanywa na serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF – katika kukabiliana na umaskini nchini.

Bwana Karas ametoa hakikisho hilo alipotembelea makao makuu ya TASAF jijini Dar es salaam na kufahamishwa juu ya utekelezaji wa Mfuko huo hususani katika Mpango wake wa Kunusuru Kaya masikini ambao pia Shirika hilo limekuwa likiufadhili.

Amesema mafanikio yaliyoanza kupatikana kwa walengwa wa Mpango huo kuanza kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali ni suala muhimu katika kuwajengea uwezo na kusaidia jitihada za serikali za kutokomeza janga la umasikini nchini kote.“Tutaendelea kusaidiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa Mpango huu unatekelezwa kwa mafanikio makubwa “ amesisitiza Bwana Karas.

Kwa upande wake ,Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bwana Ladislaus Mwamanga amemweleza Mkurugenzi Mkazi huyo wa USAID kuwa hatua kubwa imefikiwa katika kusaidia juhudi za serikali za kuwaondoa wananchi wanaokabiliwa na umasikini kwa kuwashirikisha katika shughuli za kujiongezea kipato.

“Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini wametumia fedha na elimu wanayopata kupitia TASAF kujiongezea kipato na kuboresha maisha yao” amesisitiza bwana Mwamanga.

Amemweleza Mkurugenzi Mkazi huyo wa USAID kuwa uboreshaji wa makazi, uanzishaji wa miradi midogo midogo kama ufugaji wa kuku,bata,mbuzi ,nguruwe na shughuli za kilimo ni miradi ambayo walengwa wamekuwa wakijihusisha tangu kuandikishwa kwenye Mpango.

Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF tangu mwaka 2013 na unahudumia kaya MILIONI MOJA NA LAKI MOJA zenye takribani watu milioni SITA ,Tanzania Bara ,Unguja na Pemba.
Mkurugenzi Mkazi wa USAID ,Bw. Andrew Karas (aliyevaa shati jeupe) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga juu ya utekelezaji wa shughuli za TASAF.
 Baadhi ya watendaji wa  TASAF wakimsikiliza Mkurugenzi Mkazi wa USAID wakati wa ziara hiyo aliyoifanya kwenye makao makuu ya Mfuko huo jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment