Sunday, November 12

Mchezaji wa bora wa Afrika taji la BBC mwaka 2017: Mpigie kura unayempenda

Afoty
Upigaji kura wa mchezaji atakayeshinda taji la mchezaji bora wa Afrika la BBC mwaka 2017 umeanza.
Wachezaji watano walioorodheshwa ni Pierre-Emerick Aubameyang, Naby Keita, Sadio Mane, Victor Moses naMohamed Salah.
Walitangazwa katika kipindi maalum cha moja kwa moja katika BBC.
Waliowahi kushinda tuzo hiyo awali ni pamoja na nyota wawili wa Ivory Coast Didier Drogba na Yaya Toure, Jay-Jay Okocha wa Nigeria na jagina wa Liberia George Weah.
Jopo ambalo liliwashirikisha miongoni mwa wengine Emmanuel Amuneke, mshindi wa ubingwa Afrika na Olimpiki 1996, Arnaud Djoum, mshindi wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2017 akiwa na Cameroon, na Jean Sseninde, kutoka Uganda anayechezea Crystal Palace Ladies, walikuwepo kujadili majina ya walioteuliwa kushindania tuzo hiyo.
Watano hao watakuwa wakitumai kufuata nyayo za mshindi wa mwaka jana Riyad Mahrez, aliyeng'aa mwaka 2016 akichezea mabingwa wa Ligi ya Premia mwaka huo Leicester City na Algeria.
Mashabiki wanaweza kupigia mchezaji wanayetaka ashinde kupitia ukurasa wa soka ya Afrika katika tovuti ya BBC, BBC African football, hadi upigaji kura utakapokamilika 18:00 GMT Jumatatu, 27 Novemba.
Mshindi atatangazwa moja kwa moja 17:30 GMT Jumatatu, 11 Desemba.
Pierre-Emerick Aubameyang - Gabon na Borussia Dortmund
Aubameyang: Mchezaji hatari kwa ufungaji mabao Ujerumani
Hakuna mara hata moja katika historia ndefu ya ligi kuu wa Ujerumani Bundesliga ambapo mchezaji kutoka Afrika alikuwa ameongoza kwa ufungaji wa mabao ligini peke yake hadi pale Pierre-Emerick Aubameyang alipofunga mabao 31 msimu wa 2016-17.
Idadi yake ya mabao ilimuwezesha raia huyo wa Gabon kuvunja hata rekodi iliyowekwa na mchezaji wa Ghana Tony Yeboah, ambaye alimaliza akiwa anashikilia nafasi ya ufungaji mabao ligini na mchezaji mwingine miaka ya 1990.
Kadhalika, ilikuwa ni mara ya nne kwa mchezaji kufunga Zaidi ya mabao 30 katika msimu mmoja Bundesliha - na mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 40.
Naby Keita - RB Leipzig na Guinea
Naby Keita: Mchezaji aliyewavutia sana Liverpool
Naby Keita huenda alianza msimu wa 2016-17 kama mchezaji asiye na umaarufu nchini Ujerumani, lakini alikamilisha msimu huo jina lake likiwa katika kikosi cha timu ya mwaka - kura iliopigwa ambapo mchezaji huyo wa Guinea alipata kura nyingi kushinda kiungo wa kati yeyote yule.
Klabu ya Red Bull Leipzig ndiyo iliowashangaza wengi katika msimu wa 2016-17, huku ikimaliza katika nafasi ya pili (na kufuzu katika mashindano ya vilabu bingwa), lakini ilikuwa kiungo huyo wa kati aliyeisadia timu hiyo kuwa katika nafasi ya pili.
Dakika tano tu baada ya kuchezeshwa katika kikosi cha kuanza mechi mara ya kwanza katika Bundesliga, Keita aliyenunuliwa kutoka klabu dada cha Red Bull Salzburg ya Austria, alifunga bao la ushindi dhidi ya Borussia Dortmund kunako dakika ya 89 na hivyo basi kushinda taji la mchezaji bora na timu bora ya msimu.
Kwa jumla, alifunga mabao manane, mojawapo likiwa bao lililoorodheshwa kuwania tuzo ya bao bora la msimu huku akitoa usaidizi katika ufungaji wa mabao 7.
Mchezaji huyo pia anapendwa sana kwa uwezo wake wa kurudi nyuma na kulinda lango.
Sadio Mane -Senegal & Liverpool
AFOTY 2017: Wasifu wa Sadio Mane
Nyota wa Senegal na Liverpool Sadio Mane alifanya vizuri sana mwaka 2017 hivi kwamba alipigiwa kura na wachezaji wenzake kuwa kwenye kikosi bora cha PFA.
Kadhalika, alikuwa mmoja kati ya Waafrika wawili kuteuliwa kushindania tuzo ya Ballon d'Or.
Pia alitekeleza wajibu mkubwa katika kuiongoza Senegal kufuzu kwa michuano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 2002.
Katika ufungaji wake bora zaidi akiichezea Senagal mwaka mmoja, Mane alifunga mabao manne katika mechi 9 za kimataifa.
Ilikuwa ni tofauti sana na mwanzoni mwa mwaka kwani Mane alionesha ukakamavu wake kiasi cha kufikia kasi yake ya umeme, ujanja wake na ustadi wa kutia mabao kimiani.
Baada ya kufunga katika mechi za kwanza mbili hatua ya makundi katika mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika, mwaka wa Mane ulibadilika na kuwa mchungu.
Alishindwa kufunga mkwaju wa penalti wakati wa mikwaju ya kuamua mshindi dhidi ya Cameroon na akawawezesha samba hao ambao baadaye waliibuka mabingwa kufika hatua ya nne bora. Hilo lilimdhoofisha sana Mane, machozi yakionekana kutiririka kama maji kwenye uso wake siku hiyo.
Victor Moses -Nigeria na Chelsea
Victor Moses: Mchezaji aliyewavusha Nigeria hadi Urusi
Victor Moses atakapotafakari kuhsuu maisha yake ya uchezaji, kuna uwezekano mkubwa kwamba kiungo huyo wa kati wa Nigeria na Chelsea atautazama msimu wa 2016-17 kama wakati ambao nyota ya jaha ilimuangazia.
Baada ya miaka kadhaa ya kutanga jangwani akiwa anatumwa nje kwa mkopo mara kwa mara, mchezaji huyo wa miaka 26 hatimaye alitia guu na kutulia Stamford Bridge, sana kiasi kwamba alitekeleza mchango muhimu katika kikosi kilichoshinda Ligi ya Premia.
Siku ambayo Moses ataikumbuka ni 1 Oktoba baada ya kocha wa Chelsea Antonio Conte baada ya vipigo vikali mfululizo kutoka kwa Arseanal na Liverpool alipobadili mfumo na kucheza 3-4-3 na kiungo huyu raia wa Nigeria akachezeshwa kwenye nafasi asiyoizoea pembezoni kwenye winga ya kulia kwenye mchezo dhidi ya Hull City.
Ulikuwa mchezo wake wa kwanza ligi kwake kuanza kwenye kikosi akiichezea Chelsea kwa karibu miaka mitatu. Lakini Moses alikuwa mchezaji bora na aliichangamkia sana fursa hiyo na kuonyesha mchezo wake wa kushambulia na pia kuwa mkabaji hali ikilazimu.
Ushindi dhidi ya Hull ulikuwa mwanzo wa ushindi mara 13 mfululizo kwa Chelsea kwenye ligi kuu nchini Uingereza na ukawa ni mchezo wa 22 wa Moses kuanza kwenye kikosi ligini mtawalia, hadi alipotupwa nje na jeraha kwa muda mwezi Aprili.
Mohamed Salah -Egypt & Liverpool
AFOTY 2017: Safari ya Salah kufikia ufanisi
Mohamed Salah huenda amefunga mabao chungu nzima lakini atakumbukwa nchini Misri kwa kitu kimoja- bao la dakika za lala salama dhidi ya Congo mwezi Oktoba.
Bao hilo liliwawezesha Mafirauni kufuzu kwa mara ya kwanza kwa michuano ya Kombe la Dunia baada ya kipindi cha robo karne.
Misri walifanikiwa kuwa mabingwa wa Afrika mara saba lakini walikuwa hawajawahi kushiriki katika fainali za Kombe la Dunia tangu 1990, na ikiwa katika dakika za lala salama walishinda penalti huku ikiwa matokeo ni 1-1 hatua iliyozua hisia zisizokuwa za kawaida nje na hata ndani ya uwanja.
Na mchezaji huyo ambaye alikuwa ametulia na kutobabaishwa alifunga bao hilo lililowafurahisha mashabiki wengi wa nyumbani na kumlazimu Rais Abdul Fattah Al Sisi kumpongeza kwa kuweza kuhimili shinikizo za raia milioni 80 wa Misri.
Bao hilo lilimpatia umaarufu wa kuwa mfalme wa Mafirauni 2017, huku timu hiyo ikipewa jina la utani ''Misri ya Salah'' kutokana mchezo wa kasi wa mshambuliaji huyo ambaye aliiwezesha Misri kuwika.
Kwa mfano Salah alifunga mabao matano kati ya mabao saba yaliyofungwa wakati timu hiyo ikitafuta kufuzu kwa Kombe la Dunia la Urusi.

No comments:

Post a Comment