Mbowe, ambaye ni mbunge wa Hai, alikuwa akimuhoji Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu hatua ambazo Serikali imechukua dhidi ya mauaji ya mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alphonce Mawazo, kutoweka kwa Ben Saanane, ambaye alikuwa msaidizi wake, na tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ambaye hivi sasa amelazwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
Siku chache baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Mawazo alitekwa akiwa katika kikao cha ndani cha Chadema na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa chama kimoja cha siasa, kisha kupigwa kwa silaha za jadi, na kumuua kwa kumkata kichwa kwa shoka.
Saanane, ambaye alikuwa msaidizi wa Mbowe, alitoweka siku chache baada ya kuandika makala ya kisiasa kwenye mitandao ya kijamii na hadi sasa hajulikani alipo.
Lissu alishambuliwa kwa risasi zipatazo 30 Septemba 7 mwaka huu akiwa ndani ya gari iliyoegeshwa nje ya makazi yake mjini Dodoma muda mfupi baada ya kuwasili akitokea bungeni. Pamoja na washambuliaji hao kufanya kitendo hicho mchana, Jeshi la Polisi halijaeleza hadi sasa kama limeshamkamata mtu yeyote kwa kumhusisha na shambulio hilo.
"Kumekuwa na matukio mengi yanayovunja usalama, yanayovunja amani na yanayojenga chuki miongoni mwa vyama vya siasa na kuharibu utengemano wetu wa kitaifa," alisema Mbowe.
Mbowe alisema tukio la Lissu kushambuliwa kwa risasi kwa nia ya kuua limezua hofu kubwa kwa Taifa, bara Afrika na Jumuiya ya Kimataifa.
"Nina hakika taharuki hiyo, imeharibu sana sura ya Taifa, heshima tuliyokuwa nayo kamaTaifa, na hatujaona kama Serikali inachukua hatua zozote kujaribu kufanya jambo hili lisiendelee kuharibu image (taswira) yetu kama Taifa)," alisema Mbowe.
Mbowe, ambaye chama chake kinataka uchunguzi huru wa shambulio shidi ya Lissu, alitaka kujua kama Serikali inachukua hatua zozote dhidi ya matukio hayo.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema matukio hayo yako kote nchini kuanzia ngazi familia na kwenye mikusanyiko na kwamba shambulio dhidi ya Lissu si tukio pekee.
"Hatupendi matukio haya yatokee, lakini pia utakumbuka wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiki tumepoteza watu wengi," alisema Waziri Mkuu huku wabunge wakishangilia kwa makofi na sehemu ya wabunge baada ya kutaja mauaji ya wilaya hizo tatu za Mkoa wa Pwani.
"Lakini pia hata siku za karibuni, kamanda wetu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) naye alipigwa risasi pia. Kwa hiyo tuyazungumze haya kwa ujumla wake. Na tunapoyazungumza haya kwa ujumla wake.
"Na kwa utamaduni ambao tumeujenga nchi hii katika kujilinda wenyewe kuhakikisha kwamba nchi inaendelea kuwa salama, nataka kuhakikishia kwamba vyombo vyetu vya dola vinaendelea kufanya uchunguzi wa haya.
"Na uchunguzi huu hauwezi kuwa wa leoleo halafu ukapata ufumbuzi kwa sababu wanaotenda matendo haya wanafanya mbinu nyingi za kujificha."
No comments:
Post a Comment