Thursday, November 30

Mazishi ya waliouawa maandamano ya upinzani Kenya yaandaliwa

Mashirika ya haki za binadamu yanasema watu zaidi ya 50 wameuawa tangu uchaguzi wa kwanza Agosti
Image captionMashirika ya haki za binadamu yanasema watu zaidi ya 50 wameuawa tangu uchaguzi wa kwanza Agosti
Mazishi ya baadhi ya watu wanaodaiwa kuuawa na polisi katika makabiliano kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa upinzani nchini Kenya yameanza kuaandaliwa leo.
Makundi ya Haki za Binadamu yanasema watu zaidi ya 50 wameuawa na polisi tangu uchaguzi wa Agosti, uliofutiliwa mbali na Mahakama ya Juu baada ya kesi iliyowasilishwa na upinzani.
Kisa cha hivi karibuni kikiwa cha mvulana mwenye umri wa miaka 7 ambaye aliuawa alipokuwa akicheza nje ya nyumba yake Jumanne jijini Nairobi.
Mauaji hayo yalitokea wakati wa makabiliano kati ya polisi na upinzani, siku ambayo sherehe ya kumuapisha Rais Kenyatta kwa muhula wa pili ilikuwa inafanyika.
Baadhi ya familia zilizoathiriwa zimekuwa zikipokea miili ya wapendwa wao leo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City jijini Nairobi.
Mwandishi wetu Emmanuel Igunza amekuwa huko kuzungumza na baadhi ya jamaa waliofariki ambao wanataka haki itendeke.
"Ndugu yangu Elisha Osenyo Lukuba alipigwa risasi tarehe 17 Novemba. Ni wakati wa kusikitisha sana kwetu kama familia, kwa nchi nzima kupoteza mtu huyo mwenye nguvu sana. Ni uchungu sana kuona mtu asiye na hatia akiuwawa. Serikali inayotakiwa kutulinda haitutulinda tena," amesema Geoffrey Nguyagwa Ovwiru.
Miongoni mwa viongozi ambao walijitokeza kuwaliwaza waombolezaji ni Rosa Buyu, ambaye ni Mwakilishi wa Wanawake Bungeni katika kaunti ya Kisumu, - ngome ya upinzani ambayo pia imeshuhudia maandamano na vifo.
"Hivi ni vita kwa ajili ya haki: kutaka mageuzi mazuri ya sheria za uchaguzi na watoto wenu wamelipa gharama kubwa zaidi ya maisha yao," ameambia BBC.
"Lakini tunataka kuwaambia serikali na polisi, tumechoka kulia. Tumelia sana na hatutaki kulia tena. Ni serikali ambayo inaweza kutuzuia kulia kwa sababu wanaweza kuacha uuaji huu usio na maana. Vijana hawana haja ya kufa namna hii. "
Lakini Serikali imepinga madai hayo kwamba mauaji hayo yalitekelezwa na vikosi vya usalama na kusema itafanya uchunguzi.
Katika mahojiano na Kituo cha NTV nchini Kenya, Msemaji wa Polisi, Charles Owino, alisema kuwa vifo vyote vinachunguzwa.
"Tunachukulia masuala ya vifo hivi kwa uzito mkubwa. Ni lazima tufungue uchunguzi kubaini chanzo cha vifo na kila mara ni lazima faili hiyo tuliyofungua kuwasilishwa kwa hakimu mhusika. Na iwapo afisa yeyote wa polisi atapatikana kuwa na hatia atachukuliwa hatua za kisheria," alisema Bw Owino.

No comments:

Post a Comment