Serikali ya Marekani imewataka wafanyakazi wake wote ambao hawahitajiki kuwepo ubalozini nchini Somalia, kwa wakati huu kuondoka katika mji mkuu, Mogadishu, ikieleza inatokana na vitisho maalum vilivyo elekezwa dhidi yao.
Taarifa iliyotolewa Jumamosi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inahusisha tishio hilo na kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Mogadishu, ambacho kinalindwa na Vikosi vya Umoja wa Afrika (AU) na uwanja huo unaendeshwa na kampuni ya Uturuki.
“Kutokana na taarifa ya vitisho hivyo dhidi ya wafanyakazi wa Marekani katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mogadishu, Ubalozi wa Marekani nchini Somalia umewaagiza wafanyakazi hao kuondoka Mogadishu mpaka pale taarifa zaidi itakapotolewa,” limesema tamko hilo.
Pia imewataka raia wa Marekani walioamua kubakia Somalia kuwa macho.
“Wizara ya Mambo ya Nje inawataka raia wote wa Marekani walioamua kubakia Somalia kuangalia upya mpango mzima wa usalama wenu, kuchukua hatua zinazofaa kuhakikisha usalama wenu, kuwa macho na mazingira yenu, kufuatilia vituo vya habari nchini Somalia juu ya taarifa mpya, na kuendelea kuwa waangalifu kwa kiwango cha hali ya juu,” taarifa hiyo imesema.
Wakiongea na VOA kwa sharti la kuwa wasitajwe majina, vyombo vya usalama katika uwanja wa ndege wa Somalia vimesema tishio hilo limewasilishwa kwa vyombo vya usalama na hawajui hasa tishio hilo linahusu nini hasa.
Brigedia Jenerali Abdi Ashkir Jama, ambaye ni meneja mkuu wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Adde, Mogadishu – ambao umepewa jina hilo la aliyekuwa rais wa kwanza Somalia, Aden Abdullah Osman—VOA iliwasiliana naye, lakini amekataa kuzungumza kuhusu suala hilo na kutaka iwasiliane na wizara ya usalama ya Somalia.
No comments:
Post a Comment