WAKATI makubaliano ya mwisho kati ya Kampuni ya Barrick Gold Corporation na Serikali ya Tanzania yakiwa hayajafikiwa, vigogo wawili wa kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia, wamejiuzulu nyadhifa zao.
Hatua hiyo inatajwa kuchochewa na mgogoro wa makinikia kati ya kampuni hiyo na Serikali.
Taarifa ya Acacia kwa umma jana, iliwataja vigogo hao ni Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni hiyo, Brad Gordon na Ofisa Mkuu wa Fedha, Andrew Wray, ambaye Oktoba 20, mwaka huu, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa kampuni hiyo, haitoweza kuilipa Tanzania Sh bilioni 700 ambazo Barrick Gold ilisema zitalipwa kama sehemu ya kuonyesha uaminifu.
“Hatuna huo uwezo kuilipa Tanzania ili tumalizane kwenye mgogoro wa kodi uliopo,” alinukuliwa akisema hayo wakati Acacia ilipokuwa ikiwasilisha ripoti yake ya fedha kwa robo ya tatu ya mwaka iliyoishia Septemba, iliyoonyesha kushuka kwa mapato na faida ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Licha ya Gordon na Wray kujiuzulu, taarifa ya Acacia inasema kuwa watabakia katika kampuni hiyo hadi mwishoni mwa mwaka huu ili makabidhiano ya ofisi yafanyike kwa ufanisi.
Taarifa hiyo Ilisema kuwa Gordon atarudi Australia kwa sababu za kifamilia wakati Wray anatafuta fursa nyingine kwingineko.
Tayari bodi ya kampuni hiyo imetangaza uteuzi wa Peter Geleta (54) ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Ufanisi, kuwa kaimu CEO na Jaco Maritz (42), ambaye ni Meneja Mkuu wa Fedha, ameteuliwa kuwa Ofisa Mkuu wa Fedha. Wateule hao wataanza kazi Januari Mosi 2018.
Geleta ana uzoefu wa miaka 35 katika sekta ya madini kwa nafasi zote za uendeshaji na utawala, hususani Afrika.
Taarifa ya Acacia ya jana, ilimnukuu Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Kelvin Dushnisky, akisema kuwa Gordon na Wray wamekuwa watu muhimu kwa mafanikio ya uendeshaji na fedha ya Acacia kipindi cha miaka minne.
“Kwa niaba ya Bodi na Kampuni, ningependa kutoa shukrani zetu za dhati kwao kwa mchango wao mkubwa. Tunawatakia mafanikio huko waendako. Na kwa namna ile ile tuna imani kuwa Peter na Jaco watafanikiwa katika majukumu yao,” alisema.
Mara baada ya taarifa ya Acacia kuhusu kujiuzulu kwa vigogo hao kuwekwa hadharani, Shirika la habari la Reuters kutoka London yalipo makao makuu ya Acacia, jana lilimnukuu mchambuzi kutoka asasi ya Peel Hunt, Peter Mallin-Jones akisema: “Hitimisho la wazi linaonekana ni kwamba wawili hao wanahisi kwa hali halisi ilivyo nchini Tanzania, mzozo uliopo sasa hautarajii kutatuliwa vyema au haraka.”
Hata hivyo, wachambuzi kutoka asasi ya Investec walisema kuondoka kwao kutasaidia kusafisha njia ya makubaliano na Tanzania.
“Ni wazi si jambo zuri kutokana na uzoefu mkubwa walionao Gordon na Wray, lakini hili linaweza kuituliza Serikali ya Tanzania kwa vile Barrick itakuwa na cha kueleza namna inavyotatua mambo, hata kama hayahusiani nao,” walisema wachambuzi hao.
Machi mwaka huu, Serikali ya Tanzania ilipiga marufuku usafirishaji wa makinikia nje kama sehemu ya mkakati wa kutaka kunufaika zaidi na maliasili zake.
Lakini pia Julai mwaka huu, Serikali iliwasilisha kwa Acacia bili ya dola bilioni 190 kama malimbikizo ya kodi, faini na riba kwa kiasi kinachodaiwa kukwepwa na kampuni hiyo kwa karibu miongo miwili.
WASIFU WA WATEULE WAPYA
Kabla ya kujiunga Acacia, Geleta alishikilia nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na katika kampuni ya AngloGold Ashanti kwa miaka 25 na Barrick Gold Corporation.
Alijiunga Acacia Mei 2012 kama Makamu wa Rais, Ufanisi wa Kitaasisi.
Wakati wa utendaji wake Acacia, Geleta pia alitumikia kama Meneja Mkuu wa mgodi wa Bulyanhulu na alisaidia kutengeneza muundo uliofanikiwa wa kibiashara.
Geleta ana MBA ya Utendaji kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini.
Kwa upande wake, Maritz, amekuwa na Acacia pamoja na kampuni zake zilizoitangulia tangu mwaka 2001 akishikilia nyadhifa mbalimbali za masuala ya fedha.
Awali aliajiriwa na Placer Dome, ambayo ilichukuliwa na Barrick mwaka 2006, na ilikuwa sehemu ya Acacia wakati ikianzishwa.
Mwaka 2013, alitumika miezi sita kama Kaimu Ofisa Mkuu wa Fedha kwa biashara kabla ya uteuzi wa Wray.
Maritz ni mjumbe wa taasisi ya wahasibu nchini Afrika Kusini.
Mbali ya kukaimu nafasi ya CEO, Geleta atachukua nafasi ya Gordon katika Bodi ya Wakurugenzi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Kwa msingi huo, bodi itaendelea kuwa na wakurugenzi saba, mkurugenzi mtendaji, wajumbe huru wanne wasio wakurugenzi watendaji na wajumbe wawili wasio wakurugenzi watendaji.
HALI YA BARRICK
Taarifa ya miezi mitatu ya Barrick (Julai-Septemba) iliyotolewa hivi karibuni, inaonyesha kuwa ilipata hasara ya dola milioni 11 (zaidi ya Sh bilioni 24) tofauti na faida ya dola milioni 175 (zaidi ya Sh bilioni 385) iliyopata katika kipindi kama hicho mwaka jana.
“Kupungua kwa mapato kunatokana na kushuka kwa uzalishaji na bei ya dhahabu na zuio la kusafirisha makinikia ambalo Serikali ya Tanzania iliiwekea Acacia,” inasema ripoti hiyo.
Vilevile, Barrick inasema kupungua kwa mapato yake kumechangiwa na ongezeko la makadirio ya kodi yanayofika dola 172 milioni (zaidi ya Sh bilioni 378) zilizopendekezwa katika majadiliano ya mustakabali wa operesheni za Acacia nchini.
Wakati Barrick ikitenga kiasi hicho cha kodi, Acacia ina dola milioni 128 (zaidi ya Sh bilioni 282) na kufanya jumla ya dola milioni 300 zilizokubaliwa katika mazungumzo yaliyofanyika kwa miezi mitatu iliyopita.
Katika robo hiyo ya tatu, faida ya Acacia imeshuka kwa asilimia 70 kutoka dola milioni 52.878 (zaidi ya Sh bilioni 116.331) hadi dola 16.038 (zaidi ya Sh bilioni 35.283).
Wakati wa mkutano na vyombo vya habari uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, ambaye alikuwa mwenyekiti wa wawakilishi wa Serikali, alisema Barrick wamekubali kutekeleza masharti yote ya sheria mpya ya madini.
Lakini kwenye taarifa yake, kampuni hiyo inasema itaendelea kuzungumza na Serikali ili kuondoa zuio la kusafirisha makinikia na kwamba mazungumzo hayo yataenda sambamba na kutafuta suluhu ya deni la kodi la kiasi cha dola bilioni 190 (zaidi ya Sh trilioni 424) ambazo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeitoza Acacia ikiwa ni malimbikizo ya kodi, faini na riba.
“Tunatarajia mazungumzo haya yatakamilika ndani ya nusu ya kwanza ya mwaka ujao,” inasema taarifa ya Barrick.
No comments:
Post a Comment