Sunday, November 12

Maisha ya Safiya, Mtanzania anayefanya kazi China



Hivi karibuni, mwandishi wetu RASHID KEJO alikwenda Beijing, China kuripoti Mkutano Mkuu wa 19 wa Chama cha Kikomunisti (CPC), akiwa huko alikutana na mmoja wa Watanzania 10 walioshinda shindano lililoandaliwa na kampuni ya StarTimes la kuingiza sauti kwenye tamthilia na filamu za Kichina kwa lugha ya Kiswahili, Safiya Ahmed ambaye alisimulia jinsi alivyoipata fursa hiyo na maisha yake huko China kwa ujumla.
Swali: Kwa kifupi, nieleze wasifu wako
Jibu: Jina langu ni Safiya Ahmed natokea Zanzibar. Nimeolewa na nina watoto wawili wote wa kike. Mimi ni mtoto wa nne kati ya watano na wa kike pekee katika familia yeti. Nimepata elimu ya msingi na sekondari hadi kidato cha sita katika Shule ya Laureate international na baadaye nikajiendeleza kwa kozi mbalimbali za uandishi, kompyuta na lugha.
Swali: Kabla ya kuja Beijing ulikuwa unajishughulisha na nini nyumbani?
Jibu: Nilikuwa nikiishi Zanzibar na nikifanya kazi katika Kituo cha Habari ZBC TV Karume House, zamani wakiita TVZ kabla ya kuwa shirika ila kwa sasa ni Zanzibar Broadcasting Cooperation. Ni mwandishi wa habari na mtangazaji. Majukumu yangu yalikuwa ni kutafuta habari, kusoma habari za michezo, biashara na kutangaza vipindi vya burudani (muziki), kuongoza taarifa ya habari kuruka hewani na kwenda viwanjani kutafuta habari.
Swali: Uliipataje fursa hii ya kujiunga na StarTimes?
Jibu: Kulifanyika shindano kubwa sana Zanzibar la kutafuta kipaji cha kuingiza sauti kwenye tamthilia na filamu za Kichina kwa lugha ya Kiswahili. Shindano lilitangazwa sana ila kwa vile nilikuwa na majukumu mengi kazini, sikupata habari hapo mwanzo. Nilipata habari asubuhi wakati naingia kazini saa 1:30. Nilipatwa na mshangao kuona kituoni kumejaa watu wengi nikauliza ndio nikaambiwa kuwa kuna shindano la siku moja na siku hiyo ndiyo lilikuwa linafanyika katika studio za ZBC nikasema acha nijaribu kushiriki. Nilipewa moyo wa ujasiri wa nafsi yangu kwamba nijaribu naweza.
Nikachukua fomu nikajaza nikaiwasilisha kwa wahusika papo hapo nikapewa karatasi ya mahojiano kati ya mama na mtoto wake (dialogue) nikasoma kwa hisia. Nilivyomaliza kusoma nikaambiwa nikae pembeni nitaitwa. Baadaye tukaitwa watu wengi walifika 100 waliopita kwenye mchujo wa kwanza wengine wengi walishindwa na kurudishwa. Tukaambiwa tuingie studio watano wa tano. Ilipofika zamu yangu nikaingia kwenye chumba na kuingiza sauti. Shindano lilipoisha tukatajwa washindi na mimi nilikuwa mshindi wa kwanza.
Swali: Hali ilikuwaje siku hiyo ya usaili?
Jibu: Watu walikuwa wengi sana, walifika 300, wengine walikata tamaa wakaamua kuondoka. Lakini mimi nilibaki na kwa jinsi nilivyoingiza sauti studio, nilipata bahati ya kupendwa na Wachina wenyewe. Yaani baada ya kuniona nilivyo ‘perform’ waliniita nje na kunifanyia mahojiano kwa kunirekodi na kuniuliza ukipata bahati ya kushinda utafanya nini? Uko tayari kufanya kazi nchini China nakadhalika. Hapohapo ikanijia hisia ya kushinda kwenye shindano hilo.
Swali: Safari kutoka Zanzibar mpaka China ilikuwaje?
Jibu: Nilipanda boti kutoka Zanzibar asubuhi saa moja na kufika Dar saa tatu, nikaenda moja kwa moja mpaka ofisi za StarTimes. Kufika pale nikajumuika na wenzangu tulikuwa sita. Siku hiyohiyo saa saba mchana tukachukuliwa na basi mpaka uwanja wa ndege saa 11:30 jioni tukaruka hadi Addis Ababa tukafika saa 1:45 usiku tukakaa Addis kwa saa kadhaa kufika saa nane usiku tukabadilisha ndege mpaka Beijing ambako tulifika siku ya pili saa mbili usiku.
Tulipofika tulipokewa na wafanya kazi wa StarTimes vizuri sana, yaani utadhani tulikuwa tunajuana siku nyingi kumbe tulikuwa tunazungumza tu kwa simu na baadhi yao na wengine tulikuwa hatujawahi hata kuwasiliana. Siku ya kwanza kutupokea ilikuwa raha sana. Siku ya pili tukafanya vipimo vyote vya mwili, kufunguliwa akaunti ya benki na kutengenezewa kibali cha kazi cha mwaka mmoja na mengine mengi. Siku ya tatu tukaanza mafunzo ya wiki moja na kufanya mtihani tukafaulu wote na kila mtu kuingia kwenye ofisi yake na kuanza kazi.
Tupo sita kama nilivyosema, wawili wanatoka Zanzibar wanne wanatoka Dar. Jumla ya wafanyakazi kutoka Afrika kwenye idara yetu tupo 10. Wengine wanatoka Kenya.
Swali: Hali ilikuwaje baada ya kufika China?
Jibu: Tulipofika huku kuzungumza Kiswahili ilikuwa ni mara chache sana, hadi tukutane Watanzania wenyewe kwa wenyewe ila Kiingereza ndio imekuwa lugha mama huku tulipo. Lakini ni nikienda madukani au sokoni huwa hatuwezi kufahamiana hata kidogo kwa vile wao wanazungumza lugha yao ya Kichina tu hawajui Kiingereza hapo natumia ‘goggle translater’ kutoka Kiingereza kwenda Kichina inakuwa nafuu kufanikiwa kupata unachotaka kununua.
Swali: Vipi kuhusu misosi ya huku?
Jibu: Mpaka leo sijawahi kula chakula hata kimoja cha asili cha huku na huu ni mwezi wa nane. Nikirudi kazini ndio napika mwenyewe nakula naridhika.
Swali: Tukirudi kwenye kazi yako, umejifunza nini?
Jibu: Nimepata mafunzo ambayo nayafanyia kazi kila siku. Nimefundishwa jinsi ya kutumia pro – tools ni kifaa cha ku- edit (hariri) sauti na picha kwa kutumia kompyuta ya Mac. Nimefundishwa jinsi ya kuingiza sauti ya kuunga mwenyewe na kufanya kazi kwa ufasaha kabisa.
Baada ya kumaliza mkataba wa kazi huku, nataraji kufungua ofisi yangu na kutumia ujuzi na elimu niliyoipata hapa China na sio kuiacha elimu kichwani ikapotea.
Swali: Unaizungumziaje StarTimes?
Jibu: StarTimes ni kampuni kubwa ambayo imejitosheleza kwa kila kitu na kila siku inazidi kupiga hatua kubwa mbele. Ina kila sababu ya kuchukua vipaji vipya na kuipa nguvu zaidi kampuni kwa ubora ulio madhubuti. Naishauri izidi kuwa na jicho la tatu la kuipa mabadiliko mazuri zaidi siku hadi siku kutokana na kuwa na ongezeko la watazamaji wengi katika ving’amuzi vyao na vipindi vya lugha mbalimbali vikiwa na umahiri.
Swali: Ratiba yako ikoje hapa Beijing?
Jibu: Siku za kawaida Jumatatu - Ijumaa naingia kazini saa 2:00 asubuhi na kutoka saa 2:00 usiku wakati mwingine muda wa kutoka sio maalumu inaweza ikafika saa tatu usiku kutokana na kazi zangu kuwa nyingi. Naweza kupewa mhusika mkuu akawa na lines 4,513 ukapewa deadline (muda wa kukamilisha) ya wiki moja inanibidi nikaze misuli.
Kwa wikiendi, Jumamosi naingia kazini saa 3:00 asubuhi kutoka saa 11:00 jioni. Jumapili ni siku ya mapumziko, huwa nafanya usafi, kufua, kupika vizuri na kulala sana ili kupumzisha akili kwa ajili ya kuanza kazi vizuri Jumatatu.

No comments:

Post a Comment