Na hali hii mara zote huambatana na maumivu makali kiasi cha kumfanya mtu ashindwe kabisa.
Wapo watu ambao hudai kuwa hali hiyo ya kushindwa kumeza chakula inaweza kuwakumba wale wenye tabia ya kushindwa kukitafuna kiasi cha kutosha au wanokula haraka haraka, la hasha.
Hilo siyo tatizo kubwa kwani mara tu mtu anapobadilisha utaratibu mzima wa kula chakula, hali hii huisha.
Lakini kushindwa kumeza chakula ama kumeza chakula ukiwa na maumivu, inaweza kuwa ni ishara ya tatizo fulani ambalo linahitaji ufumbuzi wa kitaalamu.
Hali hii inaweza kumtokea mtu akiwa na umri wowote. Lakini mara nyingi huwatokea watu wazima (wazee).
Kuna sababu mbalimbali zinazochangia kutokea, lakini na matibabu yake pia hutegemeana na sababu zilizofanya hali hiyo itokee.
Dalili zake
Mtu anaweza kutambua kuwa tayari analo tatizo hilo kama atakuwa anapata maumivu wakati wa kumeza chakula, kuwa na hisia kama chakula kimekwama kooni, kutoa udenda, kushindwa kutoa sauti au inyokwaruza.
Dalili nyingine ni pamoja na kurudisha chakula kinywani toka kooni, kupatwa na kiungulia cha mara kwa mara, kikohozi au kupaliwa wakati wa kumeza kinywaji au chakula.
Mtu akibaini hali hiyo, ni vema akawahi kwenda kumuona mtaalamu wa afya au daktari mapema kabla tatizo halijawa kubwa.
Kwani bila kufanya hivyo, hali hiyo inaweza kuendelea kujitokeza mara kwa mara na mgonjwa akajikuta anapungua uzito pia kwa sababu ya tatizo la kushindwa kumeza chakula kunakoambatana na kutapika.
Sababu ya kutokea kwa hali hiyo
Kumeza chakula ama kinywaji ni tukio ambalo kiutendaji ni rahisi kama msomaji unavyoweza kufanya kila siku, lakini kiutekelezaji linafanyika likihusisha vitu vingi na vinavyoweza kuingilia kati ili lisifanyike kwa ufanisi.
Kwa ujumla, hali hiyo ya mtu kushindwa kumeza chakula au kinywaji inasababishwa na mambo kadhaa.
Miongoni mwa hayo ni pamoja na uvimbe kwenye Koo ambao husababisha kipenyo cha koo kupungua.
Pia, kuwapo kwa kitu kigeni kooni. Wakati mwingine chakula au kitu chochote kinaweza kuziba koromeo. Hali hii mara nyingi huwakumba watu wazima wanaotumia meno ya bandia na watu ambao hawatafuni chakula chao vizuri.
Sababu nyingine ni kucheua mara kwa mara, kwani husababisha kuharibu koromeo kwa kuwa tindikali iliyoko tumboni huja na chakula mpaka kinywani.
Na tindikali hii huweza kuleta madhara ya vidonda kooni na kwenye koromeo na kusababisha mtu kushindwa kumeza chakula.
Saratani inavyoathiri umezaji wa chakula
Ugonjwa wa saratani ambao hutokea kwenye maeneo ya kichwani na shingoni, matibabu yake mara nyingi huathiri koo na kumfanya mgonjwa kumeza chakula.
Magonjwa ya mishipa ya fahamu
Haya husababisha mishipa ya fahamu husababisha pia mgonjwa kushindwa kumeza chakula kama itakuwa imeathirika.
Hata hivyo, licha ya mgonjwa kuweza kupatiwa matibabu, lakini anapaswa kujihadhari na sababu hatarishi zinazoweza kuchangia kutokea kwa tatizo hilo la kumeza chakula.
Sababu hizo ni pamoja na umri mkubwa. Kutokana na kukua na kuongezeka kwa umri, kawaida koo huweza kuwa kwenye hali hatarishi ya kupata magonjwa ya aina kama ya kiharusi au ujulikanao kama Parkinson.
Ndiyo maana hali hiyo ya matatizo ya umezaji wa chakula huweza kuwatokea watu wazima zaidi kuliko watu wa umri wa kati na mdogo.
Baadhi ya magonjwa yanayosababisha mtu kushindwa kumeza chakula.
Kwa watu ambao wana magonjwa yanayoshambulia mfumo wa fahamu, kadiri ugonjwa huo unavyozidi kukua hufikia hatua ya kuathiri koo na hivyo kuleta shida kwenye umezaji wa chakula.
Madhara ya tatizo hilo
Tatizo la umezaji wa chakula huweza kusababisha ukosefu wa lishe, kupungua uzito na kupungukiwa maji mwilini kwa mgonjwa na kumfanya ashindwe kupata virutubisho muhimu.
Matatizo ya mfumo wa hewa na upumuaji. Chakula ama maji yanaweza kuingia kwenye mfumo wa hewa, hivyo kuleta maambukizi kwenye mapafu au mfumo mzima wa hewa.
Matibabu
Matibabu yake huwa magumu lakini hutegemeana na ushirikiana baina ya mgonjwa na wataalamu wa afya.
Kwani mgonjwa hutakiwa kufanya mazoezi maalumu ya kumuwezesha kuifanya misuli yote inayohusika na umezaji wa chakula pamoja na mishipa yake ya fahamu kufanya kazi kwa ufanisi.
Kama mgonjwa atabainika kuwa koromeo lake lina kipenyo kidogo, daktari atalazimika kulitanua kitaalamu na vifaa ili kuondoa tatizo hilo. Tiba ya upasuaji hufanyika pale tu itabainika kuna ulazima wa kufanya hivyo ili kusafisha njia ya koromeo.
Mi nahis ninatatizo la kumeza chakula napata shida sana hata maji hayapiti
ReplyDelete