Mshtakiwa huyo ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi ndani ya kesi aliieleza mahakama jana kuwa aliteswa wakati akitakiwa kusaini karatasi ya maelezo kukiri kushiriki katika mauaji ya Msuya.
Alidai mateso hayo ni pamoja na korodani kufungwa kamba kisha kutakiwa kunyanyua tofali.
Akiongozwa na wakili wake, Majura Magafu kutoa ushahidi mbele ya Jaji Salma Maghimbi, Shaibu ambaye ni shahidi wa kesi hiyo ndogo alieleza kuwa kutokana na mateso hayo alipoteza fahamu.
Alidai kuwa mateso hayo yalikuwa na lengo la kumshurutisha akubali kusaini katika maelezo yaliyoandaliwa na polisi, yakionyesha kukiri kushiriki tukio la mauaji la Agosti 7, 2013.
Shaibu alieleza kuwa Agosti 17,2013 saa mbili usiku, alipigiwa simu na mkuu wa kituo cha Polisi Mirerani, Ally Mkalipa akimtaka afike kituoni kwa maelezo kwamba kuna jambo la kuzungumza.
Alisema alipofika kituoni, mkuu huyo wa kituo alimweleza kuwa alitakiwa ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai (RCO) Kilimanjaro, hivyo akamweka mahabusu hadi siku iliyofuata ambayo maofisa kutoka ofisi hiyo walifika.
Shaibu alidai kuwa siku hiyo alikabidhiwa kwa polisi waliotoka ofisi ya RCO, wakiongozwa na Inspekta Samwel Maimu ambaye ni shahidi wa tisa.
Alidai polisi hao walimweleza kuwa walikuwa wanatafuta simu na laini za simu na walikwenda hadi nyumbani kwake kumpekua lakini hawakupata simu walizokuwa wakizitafuta.
Alieleza kuwa badala yake, walichukua simu zake nne aina ya Nokia A220, Samsung Galaxy S4, Nokia ya tochi na BlackBerry pamoja na gari lake hadi kituo cha polisi wakisema wanakwenda kulikagua.
Alidai kuwa akiwa kituoni hapo, polisi walimfunga pingu miguu na mikono kisha wakamuingiza kwenye gari, wakamlaza kifudifudi kwenda kituo kikuu cha polisi jijini Arusha.
“Tulipofika Arusha niliingizwa kwenye ukumbi mkubwa kama hiki chumba cha Mahakama. Nilikuta polisi wenye vyeo vikubwa akiwapo RPC Arusha simjui jina na RCO Kilimanjaro, Ramadhan Nganzi.
“RPC wa Arusha aliniambia tunaomba ushirikiano wako kuhusiana na mauaji ya Erasto Msuya. Niliwaambia sijui chochote kwa sababu wakati tukio likitokea sikuwa Arusha wala Mirerani.
“Waliniambia tunakuonea huruma. Tukikukabidhi kwa hawa vijana uliokuja nao (Inspekta Samwel na wenzake) sijui kama utarudi salama. Nilisikia hofu maana ni viongozi wakubwa wa polisi,” alieleza.
Shaibu alidai baada ya kuwaambia hajui chochote kuhusu mauaji hayo, RCO Nganzi alitoa amri kwa Inspekta Samwel na timu yake kuwa waondoke naye katika ukumbi huo.
“Tulitoka tukaenda uelekeo wa Babati. Tulifika Uwanja wa Ndege wa Kisongo tukaelekea kushoto na kuishia kituo cha polisi kilichopo katikati ya mashamba makubwa.
“Waliniambia ulishawahi kusikia Guantanamo? Nikawaambia sipafahamu. Wakaniambia subiri tukiingia humo ndani utapafahamu vizuri,” alidai Shaibu wakati akitoa ushahidi wake.
Alidai kuwa kituoni hapo walimkuta polisi wa kike aliyekuwa akisikiliza redio aina ya Subwoofer ikiwa na spika zake.
Shaibu alieleza kuwa polisi aliyetajwa kuwa ni Faustine Mwafwele akaagiza (spika) zichomolewe ukutani. “Tulifika kwenye chumba kimoja ile redio wakaichomeka kwenye switch. Waliniambia wanataka kunifanyia oparesheni. Nilishangaa kwa sababu hapakuwa na vifaa vya upasuaji,” alidai.
Sehemu ya mahojiano kati ya wakili Magafu na Shaibu ilikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Magafu: Nini kiliendelea?
Shaibu: Redio ilifunguliwa, polisi ninaowatambua kuwa ni Chilumba, Samwel na Derick waliingia, wakaambiwa wanifungue pingu na kuniamuru nivue nguo zote.
Wakili Magafu: Baada ya kuvua nguo, walikwambia vitu gani?
Shaibu: Baada ya kubaki kama nilivyozaliwa, walinifunga tena pingu na kuniambia nikae sakafuni. Wakaniambia wao hawana ombi kama wale maofisa kule Arusha bali wao ni amri tu. Waliniambia hawataki maelezo wala chochote kuhusiana na kifo cha Erasto.
Wakili Magafu: Walikuwa wanataka nini?
Shaibu: Inspekta Samwel alikuwa na karatasi nyingi wala sikujua kama zilikuwa na maandishi.
Wakili Magafu: Walikwambia nini?
Shaibu: Waliniambia wanahitaji sahihi yangu tu. Niliwajibu chumba ni giza sioni hayo makaratasi. Sikuwajibu tena. Mara nikasikia napigwa na kitu kizito kichwani nikaanguka.
Wakili Magafu: Ni kitu gani kiliendelea?
Shaibu: Chilumba alinikalisha chini. Likaingizwa bomba katikati ya miguu na mikono yangu. Derick na Chilumba walininyanyua na kuniweka juu ya meza.
Wakili Magafu: Nini kiliendelea?
Shaibu: Waliniambia salama yako ni kusaini. Chilumba akachukua bomba moja akampa Derick na kumwambia “jisevie.” Hapo nilipigwa kwenye nyayo mara mbili. Nilipiga kelele lakini haikusaidia kwa sababu redio ilifunguliwa kwa sauti kubwa. Nilipoteza fahamu.
Wakili Magafu: Fahamu zilipokurudia ulitambua uko wapi?
Shaibu Nilikuwa kituo kipya kabisa. Niliuliza wale polisi wa pale maana nilikuwa na njaa na kiu ya maji, wao wakasema wameambiwa wasinihudumie chochote wala kuniambia chochote.
Wakili Magafu: Baadaye kulitokea nini?
Shaibu: Kila siku usiku alikuwa anakuja Samwel na timu yake kutoka Moshi wakinisisitizia nisaini karatasi ambazo walikuwa nazo.
Wakili Magafu: Nini ilikuwa hatima yako?
Shaibu: Siku ya mwisho nilihamishiwa Central Moshi. Nilimwambia Samwel kuwa nina njaa na kiu sana. Akaniambia tulia utakula utakaposaini. Wakati huo nilikuwa sijiwezi nilikuwa najisaidia hapo hapo.
Wakili Magafu: Ni sehemu zipi hasa uliumizwa?
Shaibu: Niliumizwa sana miguu.
(Akiendelea kutoa ushahidi wake)
Shahidi huyo alidai baadaye walimchukua na kumpeleka hadi kwenye mashamba ya miwa ya TPC usiku na kumtaka asali sala zake zote za mwisho.
Alieleza kuwa polisi aliyemtaja kwa jina la Derick, alichomoa usinge wa bunduki aliyokuwa nayo na kumchoma nao mguuni na kushindilia kwenye jeraha akimtaka asaini maelezo.
Shahidi huyo alidai kuwa baadaye alipelekwa Kituo cha Polisi cha TPC ambako maofisa wa polisi walimweleza kuwa huko atafanyiwa mateso ya mwisho.
Alidai kuwa akiwa katika kituo hicho, polisi walimning’iniza juu ya dari na kuchukua tofali likafungwa na kamba kisha kamba hiyo ikafungwa kwenye korodani zake na kuliacha likining’inia.
Mahojiano kati ya wakili Magafu na shahidi wake yaliendelea kama ifuatavyo:
Wakili Magafu: Mwisho wake ulikuwa nini?
Shaibu: Siku iliyofuata nilijikuta Central. Kuliletwa pasi ya umeme nikachomwa sehemu za miguu (akimuonyesha Jaji), walianza kunichoma hapa chini (akionyesha) baadaye wakapanda juu.
Wakili Magafu: Wakati hayo yote yanafanyika, yale makaratasi yalikuwa yamesainiwa?
Shaibu: Bado nilikuwa sijasaini.
Wakili Magafu: Kitu gani kiliendelea?
Shaibu: Pale nilikuwa naletewa maji machafu kwenye chupa ya Kilimanjaro wakinilazimisha kunywa. Yalikuwa yanawasha sana.
Wakili Magafu: Mwisho wake ulikuwa nini?
Shaibu: Niliona kweli nakufa. Nilimwambia lete nisaini.
Wakili Magafu: Ni nani alisimamia zoezi hilo la kusaini?
Shaibu: Wakati huo Koplo Seleman alikuwa ameshika Laptop. Akaniuliza umeridhika kusaini? Nilishindwa kusaini kwa sababu natumia mkono wa kushoto na vidole vilikuwa havifanyi kazi tena.
Wakili Magafu: Kwa hiyo nini kilifanyika?
Shaibu: Walinihamishia kituo cha Kiborlon. Siku iliyofuata nakumbuka ni tarehe 21 walikuja wakaniambia unatakiwa uoge tunakupeleka hospitali halafu uende mahakamani. Wakaniambia nijitahidi nisaini. Nilifanikiwa kuyasaini.
Mahakama ilipokea fomu ya polisi namba 3 ambayo aliitumia kutibiwa hospitali ya rufaa ya mkoa Kilimanjaro ya Mawenzi na cheti cha matibabu cha gereza la Karanga kama kielelezo.
Hata hivyo, wakili mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula, alimrejesha shahidi huyo Februari 10,2015 aliposomewa maelezo ya awali ya shtaka hilo.
Wakili Chavula alisema siku hiyo shahidi huyo aliiambia Mahakama kuwa alikamatwa Agosti 15,2013 na siyo Agosti 17, 2013 kama alivyotoa ushahidi wake na kumtaka aseme kama aliidanganya Mahakama.
Akijibu swali hilo, shahidi huyo alisema siku akitoa tarehe hiyo ya Agosti 15, 2013 atakuwa alisahau na kusisitiza kuwa alikamatwa Agosti 17,2013 huku akisisitiza alipata madhara makubwa ya kuteswa.
Kesi hiyo itaendelea leo, mashahidi zaidi wa mshtakiwa huyo wanatarajiwa kutoa ushahidi wao wakiwamo madaktari wa Mawenzi na Gereza la Karanga anakodaiwa kutibiwa.
No comments:
Post a Comment