Friday, November 10

KESI YA BILIONEA MSUYA: MSHTAKIWA ASEMA ALICHOMWA NA PASI YA UMEME

MSHTAKIWA wa tano katika kesi ya mauaji ya Mfanyabishara wa Madini ya Tanzanite, Bilionea Erasto Msuya, ameieleza Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, kwamba aliteswa na  polisi waliomkamata.
Katika maelezo yake   jana, mshtakiwa huyo, Karimu Kihundwa, alidai mbele ya Jaji Salma Maghimbi  kwamba alichomwa kwa pasi ya umeme kwenye visigino   akubali kusaini karatasi ya maelezo ya kukiri kosa la mauaji.
Maelezo hayo yalitolewa wakati wa kesi ndani ya kesi ya msingi ya mauaji ya bilionea huyo ambayo iliibuka baada ya kuwapo  madai ya  mateso  dhidi ya mshtakiwa huyo.
Kesi hiyo iliibuliwa na wakili anayemtetea mshtakiwa huyo,  Majura Magafu ambako upande wa mashtaka uliiomba mahakama kusimamisha kesi ya msingi na kuanza kesi ndani ya kesi  kutafuta ufumbuzi wa hoja hiyo.
Mshtakiwa Kihundwa, ambaye alikuwa ni shahidi wa kwanza katika kesi  ndani ya kesi kwa upande wa utetezi, alikuwa akiongozwa na wakili wake, Magafu.
Alidai   kabla ya kufikishwa na kusaini karatasi ya maelezo kwa mlinzi wa amani ambaye ni shahidi wa 12 katika kesi ya msingi, Ponsian Claud ambaye ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Moshi Mjini, aliteswa kwa kuchomwa na pasi ya umeme, kisha majeraha yake kuchokonolewa kwa spana ili akubali kusaini karatasi alizoletewa za kukiri kosa.
Katika ushahidi wake, mshtakiwa huyo alidai   kabla ya kuteswa hivyo akiwa katika Kituo cha Polisi Kaliua  mkoani Tabora, alipigwa magotini kwa rungu na  kitako cha bunduki.
Mahojiano kati yake na Wakili Magafu yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: Unaitwa nani?
Shahidi: Karimu Issah Kihundwa (38).
Wakili: Kabla ya kukamatwa na kuunganishwa katika kesi hii ulikuwa unaishi maeneo gani?
Shahidi: Bomang’ombe, Wilaya ya Hai , mkoani Kilimanjaro.
Wakili: Septemba 13, mwaka 2013, ulikuwa sehemu gani?
Shahidi: Nilikuwa mkoani Tabora.
Wakili: Maeneo gani?
Shahidi: Wilaya ya Kaliwa, Kijiji cha Limbuli.
Wakili: Je, huko kijijini ulikwenda kufanya nini?
Shahidi: Nilikwenda kuchimba dhahabu nikiwa na mwenyeji wangu anaitwa Ally.
Wakili: Huyo rafiki yako alikuwa ni mkazi wa wapi?
Shahidi: Bomang’ombe na alikwenda Tabora.
Wakili: Ikawaje?
Shahidi: Rafiki yangu huyo aliniongoza kwenda kwa sheikh  anayesoma dua ya mafanikio katika maisha katika Kijiji cha Limbula.
Wakili: Ieleze mahakama baada ya kufika kwa sheikh, nini kilifuata?
Shahidi: Nilibaki pale kwa sheikh kwa ajili ya kusomewa dua na rafiki yangu Ally aliondoka.
Wakili: Ukiwa pale kwa sheikh nini kilitokea?
Shahidi: Tulipokuwa tukiendelea na dua chumbani, askari walikuja.
Wakili: Walikuja kufanyaje?
Shahidi: Walimwambia yule sheikh kwamba kuna watu anawatafuta.
Wakili: Baada ya hapo ikawaje?
Shahidi: Yule sheikh aliwaambia kuna watu wametoka Moshi, hivyo aje aangalie kule ndani.
Wakili: Je, Afande Samuel alimwambia majina ya watu ambao anawatafuta?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Baada ya kumwambia aingie ndani akaangalie, ilikuwaje?
Shahidi: Waliingia ndani askari wote na kunikamata.
Wakili: Baada ya kukukamata walikupeleka wapi?
Shahidi: Walinifunga pingu mikononi na kunipeleka kwenye gari.
Wakili: Hiyo gari ilikuwa umbali gani?
Shahidi: Umbali wa hatua kama 30 kutoka pale waliponikamatia.
Wakili: Ulipofika kwenye gari walikwambia nini?
Shahidi: Walinikalisha chini na kunihoji kwa nini nilimuua bilionea Msuya.
Wakili: Ukiwa hapo  nini kilifanyika?
Shahidi: Afande Samuel aliondoka na kurudi kwa yule sheikh na baada ya muda kupita, alirudi tena na kumuamuru Afande Atwai anipige hadi niseme kwa nini nilimuua Bilionea Msuya.
Wakili: Ieleze mahakama kilitokea nini?
Shahidi: Alianza kunipiga na kitako cha bunduki kwenye magoti nikapiga kelele sana. Baadaye Afande Selemani aliingia kwenye gari na kuchukua nguo iliyokuwa kwenye begi na kunifunga mdomo  kelele zisisikike.
Wakili: Ikawaje?
Shahidi: Watu walijaa eneo lile na Afande Samwel aliamuru gari liwashwe twende kituo cha polisi.
Wakili: Ilikuwa ni kituo gani?
Shahidi: Niligundua ni Kituo cha Polisi Kaliua na baada ya kufika, waliniingiza kwenye chumba kimoja ambacho hakikuwa na mtu.
Wakili: Ikawaje?
Shahidi: Baadaye alirudi Afande Samuel na askari wengine, yaani Atwai na Selemani wakati huo nilikuwa nimefungwa pingu mikononi.
Baadaye, Afande Samuel alimuagiza askari mmoja afuate boksi kwenye gari.
Wakili: Hilo boksi lilikuwa na nini?
Shahidi: Lilitolewa pasi ya umeme.
Wakili: Hiyo pasi ililetwa kwa matumizi gani?
Shahidi: Sikujua.
Wakili: Ikawaje?
Shahidi: Baada ya hapo, Afande Samuel aliniambia nikubaliane nao.
Wakili: Ukubaliane nao kitu gani?
Shahidi: Nikawauliza kuhusu  jambo gani, Afande Samuel aliniambia najifanya sijui, wakaanza kunipiga, wakachomeka ile pasi kwenye soketi kama dakika tano hivi.
Wakili: Mbona shahidi wa awali alisema kituo cha polisi hakikuwa na umeme  ni kweli?
Shahidi: Siyo kweli kulikuwa na umeme.
Wakili: Baada ya hapo  ikawaje?
Shahidi: Walianza kunichoma nyayoni na kwenye visigino.
Wakili: Kuna sehemu gani nyingine?
Shahidi: Mikononi.
Wakili: Mbona wanasema ulikuwa na jeraha uliloungua na moto wakati ukijaribu kuwakimbia polisi?
Shahidi: Siyo kweli.
Wakili: Baada ya kukuchoma na hiyo  pasi  ikawaje?
Shahidi: Waliondoka, lakini usiku wa manane alirudi Afande Samuel  na karatasi akanilazimisha nizisaini, lakini sikuzisaini.
Wakili: Ikawaje?
Shahidi: Kesho yake tulikwenda Arusha
Wakili: Mlipofika Arusha  ilikuwaje?.
Shahid: Tulipofika kituo cha polisi, niliingizwa mahabusu, baadaye walinitoa na kunipelekeka kwenye chumba kimoja na kunipiga wakitaka nisaini zile karatasi.
Wakili: Ikawaje?
Shahidi: Sikuzisaini. Kwa hiyo, wakachuku spana, wakanivuta maganda ya vidonda.
Wakili: Nini kiliendelea?
Shahidi: Baada ya hapo, Afande Samuel alisema najidai mjanja, ila nikifikishwa Moshi nitazisaini.
Wakili: Mlifika Moshi lini?
Shahidi: Septemba 15, mwaka 2013.
Wakili: Nini kilitokea?
Shahidi: Nilipelekwa mahabusu, baadaye wakanipeleka kwa RCO Ng’anzi.
Wakili: Nini kilitokea kwa RCO?
Shahidi: Alimuuliza Afande Samuel, kama wameshanipa maagizo ili kila kitu kiende kama walivyopanga.
Wakili: Ikawaje?
Shahidi: Walinirudisha mahabusu, ila usiku walinipeleka katika chumba kimoja kwenye jengo la RCO na kuanza kunipiga ili nisaini zile karatasi.
Wakili: Je, ulisaini?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Jambo gani liliendelea?
Shahidi: Asubuhi yake walinipeleka Kituo cha Polisi Kiboriloni. Tulipofika, waliviminya vile vidonda kwa kutumia spana, lakini niliwaambia sijui chochote kuhusu hayo mauaji na baadaye walinirudisha Kituo cha Polisi Moshi.
Wakili: Ikawaje?
Sahidi: Alikuja Afande Samuel usiku na kuniambia ananipeleka kwa mkuu wake wa kazi.
Wakili: Je, ulijua huyo mkuu jina lake ni nani?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Je, mlipofika katika chumba cha mkuu wa kazi, ilikuwaje?
Shahidi: Nilikuta watu wawili akiwamo yule aliyetoa ushahidi jana.
Wakili: Ikawaje?
Shahidi: Afande Samuel alimwambia yule mkuu anipe karatasi nikaisaini.
Wakili: Hiyo karatasi wanasema ni maelezo yako uliyoyaandika mbele yake na akakusomea, ukasaini.
Shahidi: Siyo kweli.
Wakili: Je, unajua kilichomo katika hizo karatasi?
Shahidi: Sijui chochote kwani siku ya kusaini walinipa karatasi moja na hizo nyingine nimeziona hapa mahakamani.
Baada ya mahojiano hayo, wakili wa upande wa mashtaka, Omary Kibwana, alimhoji shahidi huyo na mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo.
Wakili: Kazi za madini ulianza lini?
Shahidi: Baada ya kumaliza elimu ya msingi.
Wakili: Je, mara ya mwisho kuchimba madini ilikuwa lini?
Shahidi: Mwaka 2013.
Wakili: Je, nikikwambia ulikimbia Bomang’ombe na kwenda Tabora kujificha baada ya kumuua Erasto Msuya, nitakuwa nasema uongo?
Shahidi: Ndiyo utakuwa muongo.
Wakili: Sheikh wakati anatoa ushahidi wake alisema ulikwenda kutafuta dawa kwake ili usikamatwe, ni kweli au si kweli?
Shahidi: Siyo kweli.
Wakili: Ni kweli katika ushahidi wa Sheikh Khalid alisema ulikimbia na ukakanyaga moto ukaungua?
Shahidi: Ni kweli alisema?
Wakili: Je, unataka kuiaminisha mahakama, kwamba jeraha ulilochomwa na pasi bado lipo?
Shahidi: Ndiyo.
Bilionea Msuya aliuawa Agosti 7, mwaka 2013, saa sita mchana, kando kando ya barabara kuu ya Arusha kuelekea Moshi, jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Washtakiwa katika kesi hiyo namba 12 ya mwaka 2014 ni Sharifu Mohamed, Shaibu Said, maarufu kama Mredii, Musa Mangu, Jalila Said, Sadiki Jabiri, Karim Kihundwa na Ally Majeshi.

No comments:

Post a Comment