Sunday, November 26

JPM, BUNGE WAOMBOLEZA KIFO CHA MBUNGE WA SONGEA MJINI

RAIS Dk. John Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutokana na kifo cha Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Leonidas Gama (58), kilichotokea juzi usiku baada ya kusumbuliwa kwa maradhi ya moyo.
Gama anayetarajiwa kuzikwa keshokutwa katika Kijiji cha Likuyu Fusi kilichopo Manispaa ya Songea Mjini, alikutwa na umauti katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph ya Peramiho iliyopo wilayani Songea baada ya kufikishwa kwa matibabu kutokana na kuugua ghafla.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano-Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa Magufuli ameshtushwa na taarifa ya kifo cha mbunge huyo.
“Nimepokea kwa mshtuko na majonzi taarifa za kifo cha ghafla cha Leonidas Gama, nakupa pole Spika Ndugai, wabunge na wafanyakazi wa ofisi yako.
“Kupitia kwako, naomba ufikishe salamu zangu za pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa Songea Mjini na mkoa mzima wa Ruvuma, ndugu jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu,” alisema.
Pia amempa pole Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Ruvuma, Odo Mwisho na wanachama wote kwa kumpoteza kada aliyekiwakilisha vema chama hicho katika nafasi ya ubunge.
Alisema mbali na ubunge, pia aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi zikiwamo mkuu wa wilaya na mkoa akifanya kazi kwa kujiamini na kupigania masilahi ya wananchi bila kuchoka.
Katika hatua nyingine, Ofisi ya Bunge kupitia Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, kimeeleza masikitiko yake kuhusu kifo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyomnukuu  Ndugai, ilieleza kuwa Novemba 11, mwaka huu, Gama, alirejea nchini kutoka India alikokuwa anatibiwa.
“Novemba 21 alitokea Dar es Salaam na kurejea Songea kupitia mkoani Dodoma ili kushiriki mapokezi na ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, iliyoanza jana Ruvuma,” alisema Ndugai.
Alisema Novemba 22, mwaka huu saa sita usiku aliugua ghafla na alikimbizwa Hospitali ya Peramiho kwa matibabu.
Alisema baada ya Ofisi ya Bunge kupata taarifa hizo iliandaa ndege maalumu kwa ajili ya kumsafirisha kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Alisema madaktari wa Peramiho walishauri asisafirishwe hadi hali yake itakapotengemaa lakini jana alifariki dunia.
Alisema Ofisi ya Bunge inaendelea kuratibu taratibu za mazishi ikishirikiana na Serikali na familia yake na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.
Pia taarifa kutoka Songea zinaeleza kuwa wakazi wa Songea Mjini wamepokea kwa mshtuko msiba wa Gama.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, Hamis Ally, alisema chama na wakazi wa jimbo hilo wamepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Gama kwa kuwa siku chache zilizopita alipita maeneo hayo kufanya ziara katika baadhi ya kata za jimbo hilo.
Alisema juzi usiku alipokea taarifa za ugonjwa wa mbunge huo kutoka kwa mmoja wa wanafamilia akimweleza kwamba Gama amezidiwa na homa akiwa nyumbani kwake na walifanya jitihada za kumpeleka hospitali.
“Baada ya kupata taarifa hiyo, niliondoka usiku huo saa tano na kuelekea nyumbani kwake Likurufusi na kuungana na wanafamilia kumpeleka Hospitali ya Peramiho,” alisema Ally.
Alisema baada ya kuwasili hospitalini hapo madaktari walimpeleka katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU).
Alisema kwa mujibu wa wanafamilia waliokuwa karibu naye usiku ule walimwambia kuwa Gama alitoka kuoga baada ya kuingia chumbani alianza kujisikia vibaya na alikuwa akitokwa na jasho na mwili wake kuishiwa nguvu.
Naye msemaji wa familia ya mbunge huyo, Issa Fusi, alisema mazishi yake yatafanyika keshokutwa katika Makaburi ya Likurufusi.
Kabla ya mauti hayajamkuta, inadaiwa Gama alisumbuliwa na ugonjwa wa moyo uliomsababisha kwenda India kutibiwa na safari ya mwisho alitokea huko na aliwasili hapa nchini kisha akaenda Dodoma na safari ya jimboni kwake ilikuwa ni kuiwahi ziara ya Majaliwa lakini hakufanikiwa.

No comments:

Post a Comment