Monday, November 6

JALADA LA KESI YA RAIS WA SIMBA EVANS EVEVA NA MWENZAKE BADO LIMENASA KWA DPP


Na Karama Kenyunko, Glogu ya Jamii

Kwa mara nyingine tena upande  wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva na mwenzake, umedai jalada la shauri hilo bado liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP). Aveva anashtakiwa pamoja na makamu wa rais wa klabu hiyo, Godfrey Nyange maarufu Kaburu ambapo wote kwa pamoja wanashtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter akishirikiana na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard amedai hayo leo Novemba 6, 2017 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Vitalis alidai, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba jalada la uchunguzi bado lipo kwa DPP, hivyo wanasubiri lirudishwe. Kufuatia taarifa hiyo, wakili wa utetezi, Evodius Mtawala, aliomba mahakama iusisitize upande wa jamhuri kutilia mkazo upelelezi dhidi ya shauri hilo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 10, mwaka huu, kwa ajili ya kuja kutajwa, washtakiwa wamerudishwa mahabusu

Vigogo hao wa Simba wanakabiliwa mashitaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha Dola za Marekani (USD) 300,000. Washitakiwa hao wanadaiwa  Machi 15, 2016,  walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya tarehe  wakionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa  USD 300,000 kwa Aveva wakati si kweli.

Aveva anadaiwa  Machi 15, 2016 katika benki ya CRDB, tawi la Azikiwe, lililoko  Ilala, Dar es Salaam, huku akijua alitoa nyaraka hiyo ya kughushi.

 Aveva na Nyange wanadaiwa kati ya Machi 15 na Juni 29,2016, Dar es Salaam  kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000 wakati wakijua ni zao la kosa la uhalifu la kughushi.

Aveva anadaiwa Machi 15,2016 katika benki ya Barclays, Mikocheni, Dar es Salaam,  alijipatia USD 300,000 wakati akijua zimetokana na kosa la kughushi.

 Nyange anadaiwa Machi 15,2016 katika benki ya Barclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva  kujipatia USD 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

No comments:

Post a Comment