Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi unaojulikana kama COP23, umekamilika rasmi jana mjini Bonn, Ujerumani, baada ya wajumbe kukutana kwa muda wa wiki mbili.
Wajumbe wa mkutano huo wamekuwa wakifanya vikao mbalimbali vya kutunga sheria zitakazotumiwa katika utekelezwaji wa Mkataba wa Paris, unaonuia kupunguza ongezeko la joto duniani.
Mazungumzo hayo yaliyotakiwa kumalizika jana mchana, yaliendelea hadi saa sita usiku kwa saa za Afrika Mashariki, huku mjumbe mkuu wa China, Xie Zhenhua akisema kwamba kuna masuala mengi ambayo bado yanapaswa kujadiliwa. Wajumbe wa mkutano huo wamesema mazungumzo yamekwama hasa katika masuala makuu mawili likiwemo kuhusu fedha pamoja na kuibuka tena mgawanyiko kati ya mataifa tajiri na yale yanayoendelea.
Mataifa maskini duniani ambayo ndiyo yanayokumbwa zaidi na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, yanahitaji fedha ili kujiimarisha zaidi katika kujiandaa na kujilinda na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi.
Mataifa hayo yanataka uhakika na uwazi zaidi kutoka katika mataifa tajiri kuhusu maendeleo yaliyopatikana ili kutimiza ahadi yao ya kuchangia hadi Dola bilioni 100 kwa mwaka ifikapo mwaka 2020, kama sehemu ya mkataba wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchini.
Marekani chini ya Utawala wa Rais Donald Trump ambayo pia imepunguza ufadhili katika taasisi na miradi inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi, imekuwa na misimamo mkali kawenye majadiliano ya kifedha, hatua iliyowakasirisha wajumbe wengi. Mjumbe wa ngazi ya juu wa Ulaya, Jens Mattias Clausen amesema serikali ya Trump ilishindwa kuzuia mazungumzo hayo yasifanyike, lakini hatua hiyo inaweza ikawa imechelewesha mambo. Amesema dunia inahitaji kuchukua hatua haraka.
Mazungumzo yamepiga hatua
Muda mchache kabla ya kumalizika kwa mkutano huo, Waziri Mkuu wa Fiji, Frank Bainimarama amewaambia wanadiplomasia kwamba wanapiga hatua nzuri kuhusu mkataba wa Paris na wataikamilisha kazi hiyo kwa wakati. Bainimarama ambaye aliongoza mazungumzo hayo, alikabiliwa na changamoto ngumu ya kuzipatanisha pande zinazopingana za nchi tajiri na maskini, hasa linapokuja suala la kila upande kufanya juhudi katika kuzuia mabadiliko ya tabianchi.
Wajumbe kutoka karibu nchi 200, wakiwemo wa Marekani, walikusanyika kuandaa sheria muhimu zitakazoidhinishwa mwaka ujao wa 2018 mjini Katowice, Poland kwa ajili ya kuutekeleza Mkataba wa mabadiliko ya tabianchi uliofikiwa mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015 na ambao unatarajiwa kuanza rasmi katika muda wa miaka mitatu ijayo.
Nchi zilizosaini mkataba wa Paris zinataka kupunguza ongezeko la joto duniani hadi chini ya nyuzi joto 2 za Celsius ifikapo mwishoni mwa karne. Lengo hilo halitafanikiwa mpaka nchi hizo zifanye juhudi zaidi katika kupunguza hewa chafu ya carbon inayosababishwa hasa na matumizi ya nishati inayotokanayo na vitu asilia.
Ujerumani kwa upande wake inalenga kupunguza matumizi ya gesi inayochafua mazingira kwa asilimia 40 ifikapo mwaka 2020. Serikali iliamua kuhusu namba hiyo miaka 10 iliyopita, lakini inaonekana kama mpango huo utashindikana. Kulingana na utabiri wa sasa uliotolewa na wizara ya Mazingira ya Ujerumani, nchi hiyo itakuwa na uwezo wa kupunguza matumizi ya gesi hiyo kwa asilimia 34.7 ifikapo mwka 2020.
Desemba 12 mwaka huu, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amewaalika zaidi ya viongozi 100 mjini Paris kuadhimisha miaka miwili tangu ulipofikiwa mkataba wa Paris. Trump anayetaka kujiondoa kwenye mkataba huo, hajaalikwa katika mkutano huo wa kilele uliopewa jina ''One Planet''.
No comments:
Post a Comment