Tuesday, November 14

‘Bilionea’ nyumba za Lugumi pasua kichwa


Dar es Salaam. Wanasheria wametofautiana katika sakata la Dk Louis Shika kuhusu kosa gani amefanya na sheria gani itatumika kumchukulia hatua.
Wakati wanasheria wakitofautiana polisi wamesema kuwa wanaendelea kumshikilia na kuhoji Dk Shika kabla ya kumfikisha mahakamani.
Pia wameeleza kuwa wanawasiliana na vyombo vingine vya Serikali ili kuona kama anaweza kupimwa akili.
Dk Shika alipata umaarufu kwa muda mfupi baada ya kushiriki katika mnada wa nyumba tatu za kifahari jijini Dar es Salaam na kuibuka mshindi, akiwa ameweka dau la takriban Sh2 bilioni, lakini akashindwa kufanya malipo ya awali ya asilimia 25.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya mawakili walihoji sheria gani amevunja, huku wengine wakisema alivunja sheria ya mikataba. Wakili wa kujitegemea, John Mallya alisema, “hamna jambo la jinai hapo ni suala la madai tu labda tusubiri akifikishwa mahakamani tuone atafunguliwa kesi gani.”
“Unajua katika mnada unaposema utalipa asilimia 25 unakuwa hujui hasa ni kiasi gani kwani hakuna bei rasmi, unaweza kuwa umejiandaa asilimia ya Sh500 milioni.
“Lakini inapofika zaidi ya hapo ni tatizo na ndio maana naona ni kesi ya madai ambayo Yono watakuwa wanadai kuwa kaharibu mnada, kwamba mteja wa pili angeweza kununua ila sioni jinai hapo.”
Mallya anaungwa mkono na mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk James Jesse aliyesema, “sijui ni sheria gani ambayo ameivunja katika hilo labda kama ni kuharibu mnada, waulizwe hao walioendesha watakuwa wanajua.”
Wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa alisema kilichojitokeza ni kuvunja sheria ya mikataba ambayo mteja awali alikubali kwa kufikia bei ya juu zadi ya wateja wengine. “Hakuna jinai pale na alitakiwa ndani ya saa 48 awe amefikishwa mahakakani baada ya kuwa amekamtwa au kuachiwa, lakini kama bado anashikiliwa labda kuna kitu nyuma ya pazia,” alisema Mgongolwa.
Mallya na Dk Jesse wanatofautiana na Profesa wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Cyriacus Binamungu aliyesema mara baada ya tukio hilo walikuwa na majadiliano na liliwaacha njia panda.
“Bado tunajiuliza hapo ni criminal case (kesi ya jinai) au ni nini. Mnada ni process inakuwa na taratibu zake, sasa mhusika anatakiwa kuwa aware na masharti yaliyowekwa,” alisema Profesa Binamungu
“Haitegemei mtu ashiriki kwa kuleta utani au kuvuga ili kuharibu shughuli hiyo na kama mtu anashiriki lazima afuate masharti yaliyowekwa na yule anayeendesha mnada huo.
“Haiwezekani mtu ashiriki mnada wa kwanza, pili na tatu halafu atakiwe kutoa asilimia 25 aseme hana hela. Hii nayo inatuchanganya kwani hata aliposema anaweza kufanya muamala kwa njia ya mtandao, hauwezi kuhamisha fedha Sh200 milioni, 300 au 700 kwa kutumia kadi, hapana lazima uwepo mwenyewe.”
Yono wadai alijua anachokifanya
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya udalali ya Yono, Scholastika Kevela alisema, “Dk Shika alikuwa anajua anachokifanya na kwa lengo gani.”
Alipoulizwa kwa nini hawakushtuka na kumtaka kulipa kwanza asilimia 25 kwa nyumba ya kwanza, Scholastika alisema: “ Ukiangalia baada ya kumaliza mnada wa kwanza na kwa kuwa muda wa benki ulikuwa bado, aliwekwa chini ya ulinzi kwa kushirikiana na maofisa wa TRA.
“Tangu pale na ule mnada wa pili, ili kuhakikisha hakimbii na kwa kuwa alikuwa akijieleza vizuri na alitoa nyaraka pale katika mnada wa kwanza hatukuwa na hofu, ndio maana tulivyomaliza mnada wa pili na kuhamia Upanga alibebwa na gari la Serikali na sio ajabu bila ulinzi angekimbia.”
Akijibu swali la Mwananchi kwamba mwonekano wake haukuwashtua, alisema, “katika mnada huwezi ‘kumjaji’ mtu kwa kumwona, mavazi hayampimi mtu kuwa na uwezo, niseme tu kwamba alikuwa anajua anachokifanya na kwa kuwa yupo katika mikono ya Serikali basi hatua zitachukuliwa.”
Alipoulizwa kama tukio hilo limewahi kujitokeza huku nyuma, alisema: “Hili ni tukio la kwanza, sijawahi kuendesha mnada nikakutana na kitu kama hiki.”
Polisi yaendelea kumhoji
Kaimu kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika alisema bado wanamshikilia Dk Shika na wanaendelea na uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
Kitalika alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani muda wowote baada ya uchunguzi kukamilika.
Alisema mpaka jana hakukuwa na ndugu yeyote wa mtuhumiwa huyo aliyejitokeza kushirikiana na polisi katika uchunguzi unaoendelea.
Kabla ya kumfikisha mahakamani, Kitalika alisema polisi inawasiliana na mamlaka nyingine za Serikali kuangalia kama kuna uwezekano wa kumpima matatizo ya akili.
“Bado tunamshikilia huyu mtu (Dk Shika) wakati tunaendelea na uchunguzi. Tunashauriana na taasisi nyingine za Serikali kuona kama tunaweza kumpima akili,” alisema Kitalika na kusisitiza kwamba hana uhakika ni lini mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment