Harare, Zimbabwe. Makamu wa Rais aliyefukuzwa kazi na Rais Robert Mugabe wiki iliyopita, Emmerson Mnangagwa amerejea nchini kutoka uhamishoni na ametua kwenye kambi ya Jeshi la Anga ya Manyame kwa ajili ya kuongoza serikali, shirika la habari la African News limeripoti.
Shirika hilo limeripoti pia kwamba habari ambazo lilikuwa halijathibitisha ni kwamba Rais Mugabe, mkewe Grace, na watu kadhaa mashuhuri katika siasa wamewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani.
Mnangagwa, anayefahamika kwa jina la utani la “Mamba” alifukuzwa serikalini na kwenye chama baada ya kuzuka mgogoro wa uongozi ndani ya chama tawala cha Zanu-PF kinachoongozwa na Mugabe.
Mnangagwa, veterani wa vita vya ukombozi wa Wazimbabwe kutoka kwa wakoloni weupe wachache, alikimbilia Afrika Kusini baada ya kutishiwa maisha yake.
Jeshi la Zimbabwe limechukua udhibiti wa Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC) likisema linachukua hatua dhidi ya “wahalifu” wanaomzunguka Mugabe, 93, huku likisema rais huyo na memsapu Grace wako salama.
Msemaji wa jeshi, Meneja Jenerali Sibusiso Moyo alisema hatua iliyochukuliwa na jeshi hilo hayakuwa mapinduzi. Askari, vifaru na magari yaliyosheheni silaha yalionekana yakiranda katikati ya jiji la Harare.
No comments:
Post a Comment