Tuesday, October 17

Zaidi ya Sh330 bilioni kujenga kituo cha Ubungo, kubadili mandhari Dar


Wakati ujenzi wa flyover ya makutano ya Ubungo ukiendelea, Kampuni ya Linghang Group imetenga zaidi ya Sh330 bilioni kukibadili Kituo cha Mabasi Ubungo (UBT) kuwa cha biashara.
Makubaliano yaliyofanywa kati ya kampuni hiyo, Wakala wa Barabara (Tanroads) na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) yamekamilika na kinachosubiriwa ni vibali vya ujenzi pamoja na tathmini ya athari za mazingira.
Meneja mkuu wa Linghang Group, Cathy Wang alisema endapo kila kitu kitaenda kama kinavyotakiwa basi ujenzi wa kituo hicho cha biashara kitakachojulikana kama East Africa Commercial and Logistic Centre utaanza mapema Januari.
“Tutajenga kwa miezi 15. Kitakapokamilika, kitakuwa na maduka 3,550 pmoja na eneo la kuegesha magari 5,000. Wafanyabiashara kutoka mikoani wataweza kumaliza mahitaji yao hapa hivyo kupunguza foleni ya kwenda Kariakoo,” alisema Cathy.
Wateja
Akielezea muongekano wa kituo hicho kitakachokuwa kwenye eneo la mita 124,000 za mraba na kutoa zaidi ya ajira 20,000, Cathy alisema kutakuwa na maduka ya wauzaji wa jumla na litatengwa eneo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo pia.
Kuimarisha usalama wa wateja na mali zao, alisema kutakuwa na kituo cha polisi na eneo zima litafungwa kamera za ulinzi (CCTV) huku kukiwa na nafasi za kuegesha magari chini na juu ya jingo hilo litakalokuwa la ghorofa tano.
Kurahisisha usafiri, kutakuwa na kituo cha kupakia na kushusha abiria wa mabasi ya mwendokasi huku barabara nyingine ikijengwa na Tanroads kutoka kituoni hapo mpaka Simu 2000.
Biashara
Kituo kitakuwa na huduma zote za msingi katika eneo moja. Cathy alisema kutakuwa na matawi ya benki za biashara ambayo yatawapa fursa wafanyabiashara kuweka fedha zao za mauzo hivyo kupunguza hatari ya kuvamiwa endapo wangezisafirisha kwenda kwingineko. Wateja pia wataweza kutoa fedha wanazozihitaji ndani ya jengo hilo. Kitakuwapo na ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambazo zitakuwa na dirisha moja linalotoa huduma za Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA) pamoja na nyinginezo muhimukatika kufanikisha biashara.
“Serikali itaweza kukusanya kodi na kusimamia uingizaji na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi,” alisema Cathy.
Mtandao
Ubungo haitakuwa peke yake. Itaunganishwa na vituo vingine muhimu ili kuongeza ufanisi wake. Meneja huyo alisema vituo vingine vitajengwa Kigoma Mjini na Mutukura ili kufanikisha usafirishaji wa bidha anje ya nchi.
Kufanikisha biashara, bidhaa zitapokelewa kutoka kituo cha viwanda na biashara kinachotarajiwa kujengwa Kurasini ambako wafanyabiashara watakaokuwa na maduka Ubungo watapewa kipaumbele cha kuwa na maghala ya kuhifadhia mizigo yao.
Kwa kutumia Reli ya Kisasa (SGR) inayojengwa kutoka jijini hapa kwenda mikoani, bidhaa hizo zitasafirishwa mpaka Kigoma au Mutukula kwa ajili ya masoko zilizopo ukanda huo.
Wakati Ubungo zikitarajiwa kutumika Dola 150 milioni za Marekani (zaidi ya Sh330 bilioni), Cathy alibainisha: “Kigoma Mjini tutatumia Dola 50 milioni (zaidi ya 1.1 bilioni). Miradi yote ikikamilika, Tanzania itakuwa kama Dubai au Singapore.”
Kitakapokamilika kituo cha Kigoma kitakuwa na maduka 500 yatakayokidhi mahitaji ya nchi za Burundi, Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifafanua, chaguo la kujenga kituo hicho nchini ni kuiunganisha Tanzania na nchi zisizo na bahari kufanikisha biashara kati ya ukanda huo na dunia nzima na kwamba kwa jinsi ilivyo, Tanzania itakuwa na mafanikio kama au zaidi ya Dubai ambayo imepata mafanikio iliyonayo ndani ya miongo mitatu.
Alisema kwa utafiti walioufanya Dubai, fursa zilizopo huko zipo nchini pia hivyo anaamini kukamilika kwa mradi huo kutaongeza mchango wa sekta ya biashara kwenye Pato la Taifa (GDP) na kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa.
“Kwa sasa asilimia 40 ya uchumi wa Dubai unategemea biashara, hilo litakuwapo Tanzania pia. Ubungo na matawi yake ya Kigoma na Mutukula yatasaidia kufika huko,” alisema Cathy.
Alipotafutwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori ili kufahamu utaratibu utakaokuwapo kwa zaidi ya mabasi 500 yanayokitumia kituo hicho alisema ametingwa na kutaka atafutwe leo.
“Nipigie kesho nikupe majibu ya uhakika,” alisema kwa ufupi.
Katikati ya Machi, Rais John Magufuli aliweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa barabara za juu (flyover) katika makutano ya Barabara ya Nelson Mandela inayoungana na ya Sam Nujoma, na Morogoro yaliyopo Ubungo utakaochukua miezi 30 kukamilika.
Mradi huo unajengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia ukigharimu Sh188.71 bilioni unatarajiwa kukamilika Septemba ya mwaka 2019 na kupunguza msongamano wa magari katika barabara hizo kwa kiasi kikubwa

No comments:

Post a Comment