Wednesday, October 11

WIZARA YA ELIMU YAELEZA MIKAKATI KUKUZA TEHAMA

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeeleza mikakati yake ya kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wenye malengo ya kukuza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) itakayosaidia kuzalisha wataalamu bora zaidi.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Leonard Akwilapo alitoa kauli hiyo   Kibaha jana wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Matumizi ya Tehama katika Shule za Sekondari (ADSI) utakaogharimu zaidi ya Sh bilioni nne.
Alisema lengo la kusisitiza miradi ya TEHAMA ni kuendelea kuzalisha wataalamu bora zaidi katika kuelekea uchumi wa viwanda.
Alisema dira ya Serikali ni kuifikisha nchi katika uchumi wa viwanda, hivyo jukumu lao ni kuwaandaa wataalamu mbalimbali  watakaokuwa wakisimamia na kuhudumia viwanda hivyo na kuongeza tija kwa taifa zima.
Alisema mradi huo wa ADSI, utajikita zaidi katika kujifunza kufundisha TEHAMA katika  shule za sekondari na kwa kuanzia zimechaguliwa shule 40 katika mikoa ya Pwani na Morogoro.
Alisema serikali Itahakikisha mradi huo unakuwa endelevu na katika mikoa mingine.
TEHAMA ni nyenzo muhimu katika dunia ya mawasiliano, na kwa sasa ndiyo nyenzo kuu ya utoaji na usambazaji wa taarifa kwa umma, alisema.
Aliwataka wadau wote wa elimu kuhakikisha wanafikisha stadi hizo katika ngazi za chini pia.
Meneja Mradi wa ADSI, Joyce Msolla alisema   mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, TAMISEMI na shirika lisilo la kiserikali  la Global E-Schools and Communities Initiative (GESCI).
Alisema  mradi huo utaangalia mpango endelevu wa  jumla wa shule, mafunzo ya walimu kazini, wanafunzi kupewa stadi za karne ya 21 na kuziwezesha shule kupiga hatua   ziweze kufikia umahiri wa kutumia Tehama na kuwa shule za  dijitali.

No comments:

Post a Comment