Mwijage alisema hayo jana Ijumaa Oktoba 27,2017 wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa kampuni 100 za kati zilizofanya vizuri mwaka huu. Shindano hilo huandaliwa na kampuni ya KPMG kwa ushirikiano na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kupitia gazeti la The Citizen.
Waziri Mwijage amesema hiki ni kipindi cha mpito ambacho kina mwisho na Serikali inafanya mabadiliko mbalimbali ikitaka kujua matumizi yake halisi.
“Tumekuwa hatuna uhakika wa matumizi yetu au tunachonunua. Msiwe na wasiwasi, ni kipindi cha mpito na kina mwisho wake, tutatoka. Tuwe wavumilivu tu,” alisema Mwijage mbele ya jumuiya ya wafanyabiashara waliohudhuria hafla hiyo kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Alisema lengo la kuanzisha mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano ni kujenga uchumi wa viwanda na kuleta maendeleo ya watu.
Waziri Mwijage amesema anaamini mtu mwenye shughuli ya kufanya atapata chochote.
Amesema anatambua kwamba sekta binafsi ni mhimili wa uchumi wa Taifa na kwamba, ukitaka kujenga uchumi shindani lazima uwe na sekta binafsi yenye nguvu na ushindani mkubwa.
“Jukumu langu ni kuhakikisha kwamba sekta binafsi inakuwa na ushindani mkubwa na ili kufanikisha hilo ni lazima niwasikilize ninyi,” amesema.
Waziri Mwijage pia alielezwa na wafanyabiashara hao jinsi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inavyowanyanyasa, kuwabambikia kodi kubwa na jinsi maofisa wake wanavyojipa mamlaka makubwa.
Waziri Mwijage alisema anafahamu suala hilo.
“Nalifahamu suala la manyanyaso ndiyo maana nasema tuko kwenye kipindi cha mpito. Kuna watu nawaita ‘wasiojulikana’ kwa sababu wao hawajulikani upande wa polisi wala upande wa TRA,” alisema waziri huyo.
Akiwashukuru wageni waalikwa, Mhariri Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu alisema ndani wiki mbili zijazo, gazeti la The Citizen litaandaa toleo maalumu litakalobeba maudhui ya shindano hilo.
Machumu amewapongeza waliojitokeza kushindana na washindi, akiitaka Serikali kusaidia kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu kodi kwa sababu baadhi yao wakisikia kuhusu shindano la kampuni 100 za kati wanajua kuna kuongezewa kodi.
Katika shindano hilo, kampuni 10 zilizofanya vizuri mwaka huu kwa kuanza na nafasi ya kwanza ni Dar Ceramic Centre 2001 Ltd, Songoro Marine Transport, Modern Fitting Mart Ltd, Transit Ltd, Meru Spring Water Ltd, Economic and Business Foundation Ltd, Computer and Network Technology, Premier Agencies Tanzania Ltd, Tanpack Tissue Ltd na Tahafresh Handling Ltd.
Mkurugenzi mtendaji wa Dar Ceramic Centre 2001 Ltd, Hussein Nathoo alisema siri ya mafanikio yao ni kupanua biashara. Mwaka jana ilishika nafasi ya sita katika shindano hilo ikiwa na matawi saba nchi nzima lakini sasa yapo 11.
No comments:
Post a Comment