Wednesday, October 18

WAZIRI KAMWELWE AFURAHISHWA NA UTENDAJI WA MAMLAKA YA MAJI MOSHI

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tenki la Maji la Njari.



Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira wakifungua bomba kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Maji wa Mang’ana.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amkimtua ndoo kichwani mama kutoka Kijiji cha Mang’ana, akiashiria kutimiza lengo la Serikali ‘‘kumtua mama ndoo kichwani’’ baada ya uzinduzi wa Mradi wa Mang’ana.
Msafara wa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe ukielekea kwenye Chanzo cha Maji cha Mang’ana katika uzinduzi wa Mradi wa Mang’ana.



Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe ametoa pongezi nyingi kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA) kwa kufanikiwa kutoa huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 100 kwa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Hayo aliyasema alipokuwa akizindua Mradi mkubwa wa Maji wa Manga’na, uliopo Kata ya Uru Kaskazini, utakaohudumia zaidi ya vijiji 11 katika Manispaa ya Moshi na Wilaya ya Moshi Vijijini baada ya kupokea taarifa ya hali ya huduma ya maji katika Mji wa Moshi.

“Nawapongeza MUWSA kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya, kwa kuwa ndio lengo la Serikali, kuwa ifikapo mwaka 2020 maeneo ya vijijini huduma ya majisafi na salama ifikie asilimia 85 na mijini asilimia 95. Nyinyi leo hii mmeshavuka lengo hilo kwa Manispaa ya Moshi, kwa kweli nimefurahishwa sana na jambo hili na mnastahili pongezi nyingi’’, alisema Mhandisi Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe aliendelea kusema kuwa kwa kufanikiwa lengo hilo, mamlaka hiyo sasa itaongezewa maeneo mengine zaidi, ili kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wengine wa Moshi Vijijini ambao hawajafikiwa na huduma ya maji, na kuahidi kama Waziri mwenye dhamana ya maji atawatafutia fedha kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo.

Katika hatua nyingine Mhandisi Kamwelwe ameagiza halmashauri zote nchini, kuwa usifanyike ujenzi wowote wa miradi kabla ya kupata chanzo cha maji cha uhakika, ili kuondokana na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maji nchini.

Waziri Kamwelwe alisema ni ufisadi kutengeneza miundombinu ya maji, bila kuwa na chanzo cha uhakika cha maji. Sitakubali miradi ikamilike halafu isitoe maji, wakati umefanyika uwekezaji mkubwa wa fedha za Serikali. Hivyo, ni marufuku mradi wowote kukamilika bila kutoa maji.

Naye Mkurugenzi wa MUWSA, Joyce Msiru alisema katika taarifa yake kuwa mradi huo ni moja ya miradi mikubwa iliyotekelezwa na mamlaka yake, ukiwa umegharimu zaidi ya Sh. bilioni 2 na utahudumia zaidi ya wananchi 34,000.

Mkurugenzi Msiru alitaja baadhi ya vijiji vitakavyohudumiwa na mradi huo kuwa ni Kariwa, Longuo, Njari, Rau, Okaseni na Msuni.

No comments:

Post a Comment