Dar es Salaam. Wakati Gavana Benno Ndulu akikaribia kustaafu baada ya kufanikiwa kushusha mfumuko wa bei kwa takriban miaka tisa, ubashiri wa mrithi wa katika nafasi yake kuongoza Benki Kuu (BoT) umeanza kupamba moto.
Profesa Ndulu, ambaye ni gavana wa sita tangu uhuru, atakamilisha muhula wake miezi mitatu ijayo, kulingana na Sheria ya Benki ya Tanzania ya mwaka 2006.
Tangu kutokea kwa mfumuko wa bei na kufika asilimia 20 mwaka 2011, chini ya uongozi wa Profesa Ndulu BoT imeweza kuudhibiti na kuwa chini ya tarakimu moja huku akiivusha nchi katika mdororo wa uchumi ulioikumba dunia mwaka 2008.
Ndulu pia hajaguswa na kashfa zilizoikumba nchi, hasa ya uchotwaji wa fedha kutoka Akaunti ya Escrow iliyokuwa BoT.
Ukomo wa uongozi wake ni Januari 7 na hivyo kumpa nafasi Rais John Magufuli kumteua mrithi wake.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 8 (1) cha sheria hiyo, mtu anayeshika nafasi ya ugavana anapaswa “kuwa na shahada ya kwanza ya ama uchumi, masuala ya benki, fedha au sheria, sambamba na uzoefu usiopungua miaka 15”.
Sheria hiyo pia inaweka sharti kwamba mtu huyo ni lazima “awe ameshika nyadhifa za uongozi kwenye taasisi za umma, binafsi au kimataifa”.
Tofauti na mtangulizi wake, Dk Daudi Ballali aliyehudumu kati ya mwaka 1998 mpaka Januari 8, 2008 kabla ya kutimuliwa kutokana na sakata la Akaunti ya Malipo ya Nje (Epa), Profesa Ndulu amefanikiwa kukwepa majaribu ya namna hiyo kwa muongo mzima wa utumishi wake licha ya matukio kadhaa yaliyoikumba taasisi hiyo.
Mchumi na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alisema Taifa linahitaji gavana atakayesimamia uhuru wa benki kwa mujibu wa Sheria ya BoT na si atakayefuata maamuzi ya serikali.
“Ndulu nimefanya naye kazi kwa miaka nane nikiwa mwenyekiti wa (Kamati ya Bunge ya Hesabu ya Mashirika ya Umma) PAC. Kwa pamoja tumeweza kufanya marekebisho makubwa baada ya kashfa za EPA na Meremeta na mfumo wa kusimamia deni la Taifa,” alisema Zitto.
Zitto alisema kilichomsaidia Profesa Ndulu kufanikisha utendaji wake kutoingiliwa na siasa ni “uwezo wake wa kuwaambia wakubwa hapana” na kufanikiwa kuendelea uimara wa uchumi kwa muda wa uongozi wake.
“Gavana mpya asipokuwa imara, nchi itakwenda kuzalisha noti kinyume na utaratibu na kuleta mfumuko mkubwa wa bei,” alitahadharisha Zitto.
Kuondoka kwa nguli huyo wa uchumi kunaiacha nafasi hiyo wazi kwa wasomi wawili wanaomsaidia baada ya kuteuliwa Mei mwaka huu na Rais Magufuli. Wawili hao ni Dk Bernerd Kibesse na Dk Yamungu Kayandabila. Wakati Dk Kibesse akisimamia uthabiti na usimamizi wa sekta ya fedha (FSD), mwenzake anasimamia sera za uchumi na fedha.
Mmoja kati ya wawili hao ana nafasi kubwa ya kuteuliwa endapo Rais ataamua kuwatumia watumishi waliopo katika taasisi hiyo. Sheria inampa uhuru wa kuteua mtu mwenye sifa kutoka nje ya BoT.
Dk Kayandabila alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati Dk Kibesse alipandishwa cheo baada ya kuhudumu kama mtaalamu wa masuala ya uchumi na fedha ndani ya taasisi hiyo.
Kinachotazamiwa na wengi kutoka kwa gavana ajaye ni kufanikisha lengo la Serikali kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment