Monday, October 23

Watoto walionusurika ajalini Lucky Vincent kurejea Marekani


Sioux City, Marekani. Waliokuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Lucky Vincent ya mjini Arusha, walionusurika katika ajali ya basi na kupelekwa nchini Marekani kwa matibabu, huenda wakarejea nchini humo kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Doreen Mshana, Saidia Ismael na Wilson Tarimo walirejea nchini Agosti 18,2017 wakiwa na afya njema baada ya kunusurika katika ajali iliyoua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva iliyotokea Mei 16,2017 wilayani Karatu. Hivi sasa wamemaliza elimu ya msingi shuleni Lucky Vincent.
Shirika la Siouxland Tanzania Educational Medical Ministries (Stemm) ambalo ndilo lilifanikisha matibabu ya wanafunzi hao limeanza majadiliano na taasisi kadhaa kuwezesha watoto hao kurejea Marekani kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Rais wa shirika hilo, Dk Steve Meyer amesema kwa ufadhili wao, watoto hao watajiunga na masomo ya sekondari jijini Arusha katika shule inayomilikiwa na Kanisa Katoliki nchini.
Amesema amesema yeye, mkewe na baadhi ya washirika wa Stemm watafika Tanzania Januari mwakani wakati watoto hao watakapokwenda kuanza masono.
Amesema, “Tupo katika majadiliano na taasisi kama Morningside na Briar Cliff  kuangalia namna ya kuwaleta Sioux City watoto hawa kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu,” amesema.
Wakati wakiwa Marekani watoto hao inaelezwa walivutiwa na mandhari ya mji wa Sioux kiasi cha kuonyesha hisia za kutaka kubaki huko.
Amesema watoto hao walitembezwa katika maeneo mengi na kujifunza vitu mbalimbali jambo lililowafanya wajihisi kuzoea kwa haraka mji huo.
Meyer amesema Wilson amepona kwa asilimia 95 na Sadia kwa asilimia 85, huku Doreen akihitaji mazoezi kidogo ili kukamilisha uponyaji wake. Doreen alipooza kutokana na ajali hiyo.
Watoto hao wamekuwa wakipata uangalizi wa karibu kutoka kwa wafanyakazi wa Stemm waliko nchini wakiendelea na kazi ya kujitolea.
Katika hatua nyingine, Meyer amesema yuko mbioni kuchapisha kitabu ambacho kitaelezea maajabu ya uponyaji wa watoto hao.
Amesema kitabu hicho tayari kimeanza kuandikwa na kinatarajiwa kukamilika wakati wowote kikiwa na jina la Answer the Call ikiwa na maana ya itikia wito kwa maana ya kutoa msaada kwa wahitaji.

No comments:

Post a Comment