Saturday, October 28

Watoto waliokuwa wakicheza ufukweni mwa bahari wafa maji


Zanzibar. Watoto watatu wamefariki dunia baada ya kuzama baharini eneo la Muungoni mkoani Kusini Unguja.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kheri Mussa Haji amethibitisha vifo hivyo na kuwataja watoto hao kuwa ni Issa Kombo Hassan (11), Abrahman Zahran Ali (7) na Omar Aboud (10) wote wakazi wa Muungoni.
Amesema uchunguzi uliofanywa umebaini vifo vya watoto hao vimetokana na kunywa maji mengi.
Akizungumza kwa niaba ya familia za watoto hao, Sheha wa Muungoni, Shafii Hassan amesema watoto hao walikuwa wakicheza ufukweni mwa Bahari ya Hindi.
Amesema watoto hao baadaye waliingia kwenye dau lililokuwa limetia nanga eneo hilo ambalo lilielea na wakaingia baharini pasipo watu waliokuwa karibu kujua.
Shafii amesema baada ya muda kupita ndipo watu hao walipoanza kuulizana ni wapi walipokwenda watoto hao na hawakupata jibu.
Amesema msako wa watoto hao ulianza jana Ijumaa Oktoba 27,2017 kuanzia saa 11:00 jioni hadi saa mbili usiku walipoliona dau na miili yao kupatikana chini ya bahari.
Sheha huyo amesema miili ya watoto hao imeshakabidhiwa kwa jamaa zao kwa ajili ya mazishi.

No comments:

Post a Comment