ASILIMIA 58 ya wanawake wilayani Misungwi wanaamini ni halali kupigwa na waume zao endapo watashindwa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwamo kuunguza mboga.
Hayo yalielezwa juzi na Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake Kivulini, Yassin Ally wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya programu ya kutokomeza ukatili wa jinsia dhidi ya wanawake na wasichana (GBVII).
Alisema walipoanza programu ya GBVI katika kata tano, waligundua kiwango cha ukatili katika Wilaya ya Misungwi kilikuwa asilimia 56 lakini baada ya utekelezaji kilishuka na kufikia asilimia 36.
“Kwa mujibu wa tathimini ya taifa ya mwaka 2015/16, asilimia 58 ya wanawake wilayani Misungwi wanasema ni halali kwa mwanaume kumpiga endapo ameunguza mboga, kuondoka bila kuaga na kutotunza watoto hata kama hajapatiwa matumizi,” alisema Ally.
Alisema pia katika Wilaya ya Misungwi ilibainika wananchi wengi wananyamaza wanapofanyiwa ukatili.
Hata hivyo alisema baada ya utekelezaji wa GBVI wameweza kufichua matukio mbalimbali likiwamo la polisi aliyebaka na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland, Ciaran Cannon, alisema ukatili wa jinsia uwe wa mwili, ubakaji, kujamiana, hisia au uchumi unatambulika uduniani kote na unajulikana kama moja ya ukiukwaji wa haki za wanawake na wasichana.
“Nchini Ireland ukatili wa majumbani ni tatizo, mwanamke mmoja kati ya saba ameathirika na ukatili wa mwili, ihisia au uchumi kutoka kwa mwenza wake katika maisha yake.
“Kwa Tanzania asilimia 40 ya wanawake wamekumbwa na ukatili wa mwili na mwanamke mmoja kati ya watano ameshapitia unyanyaswaji katika maisha yake,” alisema Cannon.
Alisema tatizo la unyanyasaji linasababisha gharama kubwa kwa kwa jamii, familia na nchi kwa ujumla pamoja na upatikanaji wa kipato.
Alisema ndiyo sababu serikali ya nchi yake kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Ireland imetoa fedha kwa Shirika la Kivulini kwa ajili ya kupinga ukatili wa jinsia.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema unyanyasaji wa jinsia ni jambo lililopitwa na wakati katika zama hizi na wote wanaoshiriki kuliendeleza ni washamba .
“Kwenye jamii zetu bado kuna unyayasaji lakini hili ni jambo lilitopitwa na wakati sana, kama kuna mtu bado anashiriki unyanyasaji wa watoto, wanawake na kama kuna mama anashiriki unyanyasaji wa kina baba ajijue yeye ni mshamba na amepitwa na wakati.
“Hakutakiwi kuwe na mama anayemnyanyasa baba wala baba anayemnyanyasa mama wala mtu anayenyanyasa watoto, awe wa kiume au wa kike, hatutegemei mambo haya yaendelee,” alisema Mongella.
No comments:
Post a Comment