Saturday, October 7

Wanasheria wataka mjadala wa ukomo wa umri wa rais usitishwe



Rais Yoweri Museveni.
Rais Yoweri Museveni. 
Kampala, Uganda. Kikundi cha wanasheria kimemuomba Spika wa Bunge, Rebecca Kadaga kusitisha mjadala tata kuhusu Muswada wa marekebisho ya Katiba unaolenga kufuta ibara inayozungumzia ukomo wa umri wa rais.
Wanasheria hao kutoka kampuni ya Mawakili wa Muwema  na Akampulira na Washirika wamesema mjadala wa sasa ni kuingilia uhuru wa mahakama kwa sababu mwenendo wa shauri hilo uko mbele ya Mahakama ya Katiba.
Katika barua yao ya Oktoba 3, wanasheria hao wanaomwakilisha Dk Benjamin Alipanga wamemwomba Spika Kadaga kusitisha mchakato wa marekebisho hadi hapo mahakama inayosikiliza itakapotoa uamuzi wa shauri hilo lililofunguliwa mwaka 2014.
“…Bunge haliwezi na halipaswi kujadili suala ambalo hivi sasa liko mbele ya Mahakama ya Katiba kwani kufanya hivyo utakuwa utovu dhidi ya mahakama na litakuwa kosa kwa Kanuni ya 64 ya Kanuni za Mchakato wa Bunge za mwaka 2012,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Kadhalika wanasheria hao wameiomba Mahakama ya Katiba kuharakisha kusikiliza shauri hilo ili lishughulikiwe kwa haraka.
Mwaka 2014, kupitia kwa wanasheria hao, Dk Alipanga aliyejitambulisha mwenyewe kuwa ni mpigakura na mkazi wa Paidha Mjini katika wilaya ya Zombo alishtaki katika Mahakama ya Katiba chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) na wajumbe wa Kamati Kuu (CEC).
Walioshtakiwa katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu Justine Kasule Lumumba, naibu wake Richard Todwong, mwekahazina Rose Namayanja na naibu wake Kenneth Omona. Wengine ni mwanasheria mkuu na tume ya uchaguzi.
Katika shauri hilo pamoja na mambo mengine, Dk Alipanga anapinga hatua ya chama cha NRM na CEC kuanzisha mchakato wa marekebisho ya Ibara ya 102, 105 na 107 za Katiba kwa lengo lakuondoa ukomo wa umri wa rais wa miaka 75.
Inadaiwa kwamba lengo la marekebisho hayo ni kumnufaisha mtu mmoja tu Rais Yoweri Kaguta Museveni jambo ambalo ni kinyume cha katiba.
“Nimeshauriwa na wanasheria wangu na kwa hakika naamini hivyo kuwa ni kweli kwamba vitendo vinavyolalamikiwa hapa vinakwenda kinyume cha katiba na ikiwa walalamikiwa hawatazuiwa watasababisha ufashsti, kutoadhibiwa, vurugu zinazoweza kudhuru mwili mambo ambayo mwisho wake yatazonga badala ya kulea na kuendeleza mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na utawala wa sheria,” kinasomeka kiapo cha Dk
Kwa mujibu wa barua hiyo, moja ya ya maombi ya Dk Alipanga ni mahakama kuweka zuio la kudumu dhidi ya Bunge lisifanye marekebisho au kwa namna yoyote isichezee au kujaribu kuchezea vifungu mbalimbali vya Katiba zikiwemo Ibara 1,2,3, 8A, 20, 21, 28, 43, 44, 71,72,79, 98,99, 102, 103,105, 106 na 107.
Nakala ya barua hiyo alipelekewa naibu Jaji Mkuu na kuwekwa kwenye faili siku hiyohiyo Muswada wa Marekebisho ulipowasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza.

No comments:

Post a Comment