Kwa sasa Kenya ipo katika kipindi cha vurugu za kisiasa, zikitawaliwa na maandamano tangu Mahakama ya Juu ifute uchaguzi wa Rais baada ya kubaini ukiukwaji wa taratibu.
Umoja wa wapinzani, Nasa ambao ulifungua kesi hiyo umekataa kushiriki marudio ya uchaguzi na sasa wafuasi wake wanaendesha maandamano yanayosababisha mapambano na polisi.
Jana katika maonyesho ya siku tatu ya kimataifa ya utalii yanayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC), baadhi ya wadau wa utalii na mawakala walisema idadi ya watalii imeongezeka kwasababu wanaogopa kwenda Kenya.
“Watalii wengi wanasema hupendelea kwenda Kenya kwa sababu ya miundombinu yao ni mizuri na unafuu wa gharama za utalii. Lakini sasa wanahofia usalama wao kutokana na hali ya kisiasa iliyopo,” alisema Francis Lohay, mkuu wa fedha wa kampuni ya Bougain Villea Safari Lodge.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya kitalii ya Patamu Lodge, Raymond Massae alisema kwa sasa watalii hawapendelei kwenda Kenya, hivyo ni fursa kwa wadau wa ndani lakini Serikali inapaswa kuongeza utangazaji wa vivutio vya utalii na sio kutegemea anguko la wengine.
“Kwa kujitangaza zaidi tunaweza kuendelea na kasi hii au kuongeza idadi ya watalii kwa sababu nchi hii ina vivutio vingi na vya kipekee. Kinachokosekana ni kuvitangaza kwa nguvu,” alisema Massae.
Juzi, mkurugenzi mtendaji wa Tanapa, Allan Kijazi alisema mapato yatokanayo na utalii kwa mwezi wa Julai na Agosti yamevuka lengo lililowekwa kwa asilimia saba.
Alisema mapato yaliyotarajiwa ni Sh70 bilioni lakini walikusanya Sh75 bilioni hivyo matumaini ya kufikia malengo ya mwaka ni makubwa.
Kuhusu mwenendo huo, waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Khamis Kigwangala aliungana na wadau wa sekta ya utalii kusema kuwa utalii nchini unakwenda vizuri kutokana na baadhi ya washindani kutokuwa na hali nzuri inayovutia kwa sasa.
“Watalii ni wengi mpaka hoteli zetu zinashindwa kuwamudu,” alisema waziri huyo.
“Hii ni kutokana na baadhi yao kuchagua kuja hapa na si kwa wenzetu. Sasa tunafanya uhamasishaji wa sekta binafsi kuwekeza katika hoteli hususani za kitalii,” alisema Dk Kigwangala.
No comments:
Post a Comment