Tuesday, October 3

Uongozi Kilimanjaro watembelea nyumba zilizowekwa X na Rahco



Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira 
Moshi. Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro inatembelea eneo la Pasua kitalu JJJ ambako nyumba zaidi ya 70 zimewekwa alama na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) kwa ajili ya kubomolewa.
Kamati hiyo ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira imetembelea eneo hilo kutokana na wananchi kutoa malalamiko kuhusu nyumba zao kuwekwa alama za X.
Viongozi wa kamati hiyo  wamefuatana pia na wapimaji, maofisa wa ardhi na wa mipango miji.
Wamiliki wa viwanja katika eneo hilo wanalalamika kuwa wa hati miliki zilizotolewa na mamlaka halali, walipatiwa vibali vya ujenzi na kulipia viwanja vyao kodi ya majengo na ya pango.
Kwa mujibu wa wananchi hao waligawiwa eneo hilo na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kati ya mwaka 2005 na 2010 baada ya eneo hilo kubadilishwa matumizi na kuwa la makazi.
Wananchi hao wameeleza mwaka 1962 eneo hilo lenye viwanja 90 lilipendekezwa kupitishwa reli ambayo ingehudumia viwanda ambavyo hata hivyo havikujengwa.
Taarifa zinasema mwaka 2002 halmashauri iliomba kubadili matumizi ya eneo ambalo lilipangwa kupita reli ombi linaloelezwa kuwa liliridhiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Rahco Septemba 14 iliwapa wananchi waliogawiwa viwanja hivyo notisi ya kubomoa nyumba zao katika eneo hilo.
Mkazi wa eneo hilo, Japhet Mmbaga amesema wao si wavamizi bali waligawiwa kihalali na mamlaka za Serikali, hivyo si haki kuvunjiwa nyumba zao bila kufidiwa.
Wiki iliyopita mkuu wa mkoa, Mghwira aliiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kukutana na Rahco ili kutatua mgogoro huo.

No comments:

Post a Comment