Saturday, October 28

Ulimwengu ashangaa wizara inavyofungia vyombo vya habari

Mwandishi wa habari wa siku nyingi, Jenerali
Mwandishi wa habari wa siku nyingi, Jenerali Ulimwengu      
Dar es Salaam. Mwandishi wa habari wa siku nyingi, Jenerali Ulimwengu amesema anashangaa kuona kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ni kufungia vyombo vya habari kama magazeti na redio vinapokosea badala ya kuwa mlezi kwa vyombo hivyo.
Amesema katika Taifa linalohubiri na kufuata misingi ya kidemokrasia huwezi kuona wizara ikitoa adhabu ya kuvifungia vyombo vya habari ambavyo wakati mwingine huteleza katika kazi zao kwa bahati mbaya.
Aliitaka wizara hiyo kuwa mlezi kwa vyombo vya habari na kujielekeza katika kutoa miongozo na siyo kuchukua jukumu la kuyafungia magazeti yanapojikwaa kwenye taaluma zao.
“Hii wizara inapaswa kufanya kazi ya uelekezaji wa Taifa na siyo kama tunavyoona hapa kufungia magazeti tu. Simaanishi kwamba ndugu yangu (Harrison) Dk Mwakyembe asiwe na kazi laa ...inatakiwa kuwe na wizara ambayo itakuwa ikitoa mwongozo kama ilivyo kwa wenzetu,” alisema Ulimwengu wakati akizungumza kwenye mdahalo uliofanyika jana katika Makumbusho ya Taifa.
Mdahalo huo ulioandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle (DW), ulikuwa ukijadili mada isemayo ‘vyombo vya habari dhidi ya taarifa za uongo.’
Baadhi ya wazungumzaji kwenye mdahalo huo walikuwa ni pamoja na Dk Mwakyembe, Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Dk Ayoub Rioba na mmiliki wa mtandao wa Jamii Forum, Maxence Mello.
Akijibu hoja ya Ulimwengu, Waziri Mwakyembe alisema kasumba ya Watanzania wengi ni kutekwa na utamaduni wa nchi za Magharibi kiasi kwamba hata jambo baya likifanywa na kiongozi wa nchi linaonekana zuri lakini jambo kama hilo likafanywa na kiongozi wa Tanzania basi itaonekana kuwa nongwa.
“Unajua Mwalimu Nyerere alitufundisha kuwa ili Taifa liendelee linapaswa kuwa na vitu vinne; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora lakini hapa sasa watu wameongezea vitu vitano; watu, ardhi, siasa safi, uongozi bora na Mzungu,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza, “Ndugu yangu Ulimwengu amehoji sisi tukikosewa tunaadhibiwa na nani, sisi tukikosea tunapigiwa kura haturudi serikalini.”     

No comments:

Post a Comment