Friday, October 6

UCHAMBUZI: Tutafakari utekelezaji wa usawa wa kijinsia



Lilian Timbuka

Lilian Timbuka 
Nilipokuwa natafakari kuhusu mada aliyoitoa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake katika Maendeleo na Mawasiliano Afrika, na Mtandao wa mashirika yanayofuatilia utekelezaji wa mkataba wa hiyari wa jinsia na maendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Emma Kaliya aliyoitoa hivi karibuni kwenye Tamasha la Jinsia lililomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, nilijiuliza maswali mengi, mojawapo ni la Wanawake wa Tanzania kama wanaweza kufanya tathimini ya jumla juu ya hali halisi ya usawa wa kijinsia tangu 1996?
Jibu nililolipata ni ndiyo. Kwani Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, ipo kwenye kipindi cha kujitambua na kutafakari, kasi ya kutaka kuleta usawa wa kijinsia miongoni mwa jamii inaongezeka. Kwani tayari tunashuhudia namna asasi nyingi zinazotetea haki ya mwanamke na mtoto zinavyopambana kutaka hali hiyo izingatiwe kwenye ngazi zote za jamii.
Kuna usemi usemao “Kisicho tambulika hakithaminiwi.” Usemi huu unaakisi hali yetu nchini. Ukichunguza, licha ya nchi kupiga hatua kidogo kwenye nyanja ya usawa, bado kuna vikwazo katika utekelezaji wa ajenda hiyo.
Kwani bado kuna mkwamo wa utekelezaji wa baadhi ya vipengele vilivyoainishwa na Mkutano wa Mkuu wa Beijing uliofanyika takribani miaka 22 iliyopita. Yapo maeneo muhimu yanayoonyesha hakuna nchi hata moja hadi sasa iliyoweza kufikia malengo hayo tangu watia saini walipopitisha azimio hilo. Tamko la Ulingo wa Beijing liliweka agenda na maazimio kwaajili ya kuinua malengo ya usawa, maendeleo na amani kwa wanawake wote kila mahali. Nchi nyingi Tanzania ikiwamo, bado zina msukumo unaorudisha nyuma upatikanaji wa haki za wanawake kutokana na sheria kandamizi zinazoshindwa kutambua hatua zilizopigwa na wanawake. Kaliya akizungumza kwenye Tamasha la Jinsia lililofanyika katika Viunga vya Ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) hivi karibuni, alisema bado kuna mambo yanayorudisha nyuma juhudi zinazofanywa na Serikali na wadau wanaotetea haki za Wanawake na watoto. Alitolea mfano wa kuminya uhuru wa kujieleza na kutoa mawazo, jambo alilosema linaleta madhara makubwa kwa wanawake hasa katika kuchagua haki zao za uzazi salama.
Hata hivyo, pamoja na mambo yote, anasema haki za kiuchumi za wanawake zinabakia kuwa kipaumbele cha juu katika ajenda ya dunia. Kwa mfano, Tume ya Haki ya Wanawake (CSW 61) mwaka huu, ilijikita kuzungumzia ulimwengu wa kazi na imebainisha kuwapo kwa ongezeko la tofauti za kijinsia katika ujira, madhara yanayotokana na kazi zisikuwa na kipato zifanywazo na wanawake na wasichana. Mkutano wa jopo maalumu kuhusu Maendendeleo Endelevu ulio hitimishwa hivi karibuni ambao Lengo la 5 juu ya kuendeleza Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake lilifanyiwa mapitio, ulibainisha uhitaji wa takwimu za kijinsia katika sera na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuweza kuyafikia malengo husika. Hali hiyo ilizifanya nchi sita za Afrika kwa hiyari yao, zikawasilisha ripoti wakati wa mkutano mkuu wa Jukwaa la Siasa, Julai mwaka huu zikiwa na lengo la kutaka kusonga mbele. Ajenda kama hizo, Tanzania tunapaswa kuzisimamia ili wanawake nao washiriki katika michakato ya ngazi ya kitaifa, kikanda na hata kidunia ili kumletea mwanamke wa ki-Tanzania mabadiliko ya kweli. Mwaka 2010, Wakuu wa Nchi za Afrika walitangaza 2010 hadi 2020, ni muongo wa wanawake wa Kiafrika na 2015 hadi 2016, Umoja wa Afrika (AU) ulijikita kushughulikia haki za wanawake, hali hii ilithibitisha wazi kuwa utashi wa kisiasa sasa ni kuweka agenda ya haki za wanawake kama kipaumbele cha juu katika muundo wote wa AU.
Naamini Tanzania bado inahangaika kukabiliana na tofauti zilizopo kwenye usawa wa kijinsia kama ilivyo kwa nchi nyingine. Ndiyo maana makongamano kama ya Tamasha la Jinsia lazima yaendelezwe ili kusaidia kupaza sauti. Kwa mujibu wa Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Haki za Watu, ni nchi 36 pekee zimetia saini na kuridhia mikataba hiyo. Zingine 15 zimetia saini na tatu hazijatia saini kabisa.

No comments:

Post a Comment