Saturday, October 14

SERIKALI YATEKELEZA AMRI YA MAHAKAMA YA KUMPELEKA HARBINDER SINGH HOSPITALI YA MUHIMBILI KWA MATIBABU


Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii

Upande wa Jamhuri umetekeleza amri iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kumpeleka  mmiliki wa IPTL, Harbinder Singh Sethi kutibiwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili 

Wakili wa serikali, kutoka Takukuru, Leornad Swai ameeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Huruma Shaidi na kuongeza kuwa, mshtakiwa alifanyiwa vipimo na atapelekwa tena hospitalini hapo kuchukua majibu baada ya wiki moja. 

Sethi ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya uhujumu Uchumi anashtakiwa pamoja na  James Burchard  Rugemarila ambapo wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi ikiwemo  kutakatisha fedha na kuisababisha serikali hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Baada ya taarifa hiyo Wakili wa utetezi Respicius Didas alilalamikia kucheleweshwa kwa upelelezi na kudai kuwa washtakiwa walifika mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 19 kipindi chote hicho wamekuwa wakiteseka kwa kukaa ndani na upande Wa Jamuhuri kila wakija wanasema upelelezi bado na kuongeza kuwa wateja wake kuendelea kuwa ndani kinaathari ndani yake.

Akijibu hoja ya kuchelewa kukamilika kwa upelelezi,  wakili Swai amedai, kesi inayowakabili watuhumiwa ni ya kughushi ambayo upelelezi wake unachukua muda mrefu na sheria iko wazi kwa hilo lakini tutajitahidi kukamilisha upelelezi.

No comments:

Post a Comment