Naibu wa rais wa Kenya William Ruto amesema kuwa hakutakuwa na tatizo lolote ikiwa tume huru inayosimamia uchaguzi nchini humo IEBC itayatimiza matakwa yaliyotolewa na upinzani NASA ilimradi uchaguzi ufanyike.
Naibu wa rais wa Kenya William Ruto amesema kuwa hakutakuwa na tatizo lolote ikiwa tume huru inayosimamia uchaguzi nchini humo IEBC itayatimiza matakwa yaliyotolewa na upinzani NASA kuelekea katika uchaguzi mpya wa rais. Kando na hilo, muungano wa upinzani NASA umeahirisha maandamano yake kwa siku ya leo ili viongozi kuwatembelea waathiriwa waliojeruhiwa katika maandamano ya jana waliolazwa hospitalini.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi, naibu wa rais nchini Kenya William Ruto amesema kuwa Ikiwa tume ya uchaguzi itaamua kufanya mazungumzo na washindani wao kuhusu kuwafuta kazi baadhi ya maafisa wa tume hiyo au kuwabadilisha washirika wa tume hiyo wanaowapa vifaa vya uchaguzi, kwa dhamira ya kuwezesha uchaguzi kufanyika, basi watashiriki. "Wanaweza kukubaliana kuhusu lolote, wakikubali kuhusu kampuni mpya ya kuchapisha karatasi, kampuni mpya ya kutoa mitambo ya uchaguzi, kumfuta kazi Chiloba, yote hatuna shida. Tuliambia IEBC kuwa chochote watakachokubaliana na washindani wetu, sisi hatuna shida nacho." Amesema Ruto.
Ruto amemlaumu Odinga kwa kujaribu kusababisha machafuko kupitia njia ya maandamano na kudai ni njama yake ya kutaka kujumuishwa kwenye serikali ya muungano, hatua ambayo upande wa Jubilee haiko tayari kukubali.
Hata hivyo madai kama hayo pia yamepingwa vikali na Raila Odinga, aliyesema mnamo Jumapili kuwa hawapo tayari kwa mpango huo, maarufu nchini Kenya kama serikali ya Nusu Mkate.
Utata kutokana na Raila kujiondoa katika uchaguzi
Ruto ameongeza kuwa njama hiyo ya kisiasa ni sharti ipingwe. Ruto amesema "walitaka uchaguzi kurudiwa, ukakubaliwa, na sasa hawataki kushiriki, wanataka nini?"
Odinga amejiondoa kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kurudiwa Oktoba 26, akisema tume ya uchaguzi imeshindwa kutimiza masharti waliyowasilisha kwao ili kuwezesha uchaguzi wa haki. Kama njia ya kushinikiza kutimizwa kwa masharti hayo ya kuleta mageuzi katika tume ya uchaguzi Raila aliitisha maandamano ya kila siku.
Lakini upinzani umeyaahirisha maandamano hayo kwa siku moja ili kuwawezesha kuwatembelea wafuasi wao waliolazwa hospitalini baada ya kujeruhiwa katika maandamano ya awali. Maafisa wa NASA wanailaumu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji. Ripoti ya mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za kibinadamu, Amnesty International na Human Rights Watch ilisema polisi waliwaua kati ya watu 33-50 kufuatia maandamano yaliyozuka punde baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa Agosti nane.
Kando na hayo ni kuwa mahakama kuu imeifuta kwa muda marufuku iliyotolewa na serikali kupinga maandamano katikati ya miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu.
Aidha zipo takriban kesi tano ambazo zimewasilishwa mahakamani zinazofungamana na uchaguzi huo. Baadhi zikitaka tume ya uchaguzi ilazimishwe kuuahirisha uchaguzi huo hali ambayo imezidi kuwaacha Wakenya wengi na maswali kuhusu utayari wa kufanyika kwa uchaguzi mpya wa rais.
Mahakama ya Juu: Huwezi kuyabadilisha matokeo.
Mahakama ya juu nchini humo leo imetoa uamuzi mwingine kuhusiana na matokeo ya uchaguzi. Mahakama hiyo imesema mwenyekiti wa tume ya uchaguzi hawezi akayafanyia marekebisho matokeo ya uchaguzi ambayo yamewasilishwa katika kituo kikuu cha kuhesabu kura.
Uamuzi huo unafuatia ombi lililowasilishwa na mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati, kutaka ufafanuzi wa kisheria kuhusu wajibu wake katika kuhakiki matokeo ambayo yamewasilishwa kutoka maeneo bunge hasa endapo yana tashwishi.
Tume inayosimamia uchaguzi imeshikilia kuwa itaandaa uchaguzi jinsi ilivyopanga kufanyika tarehe 26 Oktoba, lakini kujiondoa kwa kiongozi wa muungano wa upinzani wa NASA Raila Odinga ambaye pia ndiye mgombea mkuu dhidi ya rais Uhuru Kenyatta, kumeibua wasiwasi wa utata wa kisiasa.
Kulingana na katiba ya Kenya, uchaguzi unaorudiwa sharti ufanywe ndani ya muda wa siku 60 baada ya matokeo kubatilishwa.
No comments:
Post a Comment