Friday, October 13

ROMANUS MWANGI’NGO: UZAGAAJI WA MAJITAKA UTAKUWA HISTORIA

SERIKALI kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji inaendelea kuboresha hali ya usafi wa mazingira kwa kuongeza uwezo wa mfumo wa ukusanyaji na usafishaji wa majitaka katika jiji la Dar es Salaam.
Maandalizi ya awamu ya kwanza ya mpango huo yameanza baada ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) kukabidhiwa eneo la Jangwani ambapo mtambo wa kwanza wa kisasa wa kusafisha
majitaka utajengwa.
Mradi huu ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuongeza uwezo wa mfumo wa ukusanyaji na usafishaji wa majitaka katika jiji la Dar es Salaam ambapo lengo ni kulaza kilometa 563 za mabomba ya ukubwa mbalimbali ya ukusanyaji majitaka yatakayokusanya majitaka na kuyamwaga katika mitambo mikubwa mitatu itakayojengwa Jangwani,
Kurasini na Mbezi.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangi’ngo, anasema mitambo hiyo mipya itatumika kuzalisha gesi asilia na umeme kwa ajili ya kujiendesha, hivyo kupunguza matumizi na gharama
za umeme kwenye mradi huo.
Anasema maji yatakayokuwa yamesafishwa yatauzwa na kutumika katika shughuli mbalimbali kama vile kupozea mitambo na umwagiliaji na tope litakalobaki baada ya mchakato huo wa usafishaji litatumika kama mbolea kwa ajili ya kilimo.
Katika eneo la Jangwani, bustani ya kisasa itakayokuwa na miti ya kivuli, maua na viti vya kupumzikia itatengenezwa ili kuboresha taswira ya eneo hilo.
Mwangi’ngo anasema mradi huo unahusu ujenzi wa mtambo wa kusafisha majitaka eneo la Jangwani na utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kusafisha mita za ujazo 200,000 kwa siku.
Mfumo wa mabomba yenye urefu wa kilometa 376 yatakayolazwa kuanzia Ubungo hadi Jangwani, Kinondoni, Mwananyamala, Msasani, katikati ya jiji na Ilala utajengwa.
Awamu ya kwanza ya ujenzi itahusisha mtambo utakaoweza kusafisha mita za ujazo 25,000 za majitaka kwa siku na mabomba ya kilometa 17.43 yatakayojengwa katika mitaa ya eneo la Magomeni.
Katika awamu hii ya kwanza bomba linalomwaga majitaka baharini litaacha kutumika na badala yake majitaka hayo yatakwenda kusafishiwa katika mtambo huo.
Kuhusu mfumo wa majitaka Mbezi Beach, Mwang’ingo anasema mradi huo unahusu ujenzi wa mtambo wa kusafisha majitaka utakaojengwa eneo la Kilongawima ambapo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kusafisha mita za ujazo 16,000 kwa siku na utajumuisha mfumo wenye urefu wa kilometa 97 utakaojengwa katika eneo la Mbezi Beach, Kawe, Kilongawima, Tegeta na maeneo mengine jirani.
Mradi huo utajengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia kupitia mkopo wa masharti nafuu na unatarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 65.
Anasema utaratibu wa kumtafuta mkandarasi mshauri atakayefanya usanifu wa kusimamia ujenzi ulianza Februari mwaka huu na ujenzi unatarajiwa kuanza mapema mwakani.
Mradi mwingine ni ujenzi wa mfumo wa majitaka Kurasini utakaojengwa katika maeneo yalipo mabwawa ya kusafisha majitaka.
Anasema mradi huo utakuwa na mfumo wenye urefu wa kilometa 90 utakaolazwa katika maeneo ya Keko,
Chang’ombe, Kurasini, Temeke na Uwanjawa Taifa. Mtambo huu utakuwa na uwezo wakusafisha mita za ujazo 11,000 kwa siku.
Awali katika utafutaji wa eneo la Jangwani, mamlaka iliomba kutumia eneo hilo baada ya kupata kibali kutoka Manispaa ya Ilala.
Baada ya notisi kutolewa Agosti 16 mwaka huu, kazi ya usafishaji wa eneo hilo ilifanywa na manispaa na kulikabidhi
rasmi kwa mamlaka.
Meneja Uhusiano wa Jamii wa DAWASA, Neli Msuya, anasema mradi wa uboreshaji wa huduma zanugawaji na usambazaji maji unaendelea kutekelezwa kwa kasi katika maeneo mbalimbali jiji la Dar es salaam na katika miji ya Bagamoyo na Kibaha.
Mradi huo ulianza rasmi Machi mwaka 2016 na utakamilika Novemba 2017, ambapo kazi zinazofanyika chini ya mradi huu ni pamoja na ujenzi wa matanki tisa ya kuhifadhi na kusambaza maji yenye ukubwa wa kuhifadhi lita
milioni 3 hadi milioni 6, ujenzi wa vituo vinne vya kusukuma maji, ununuzi na ufungaji wa pampu kubwa za kusukuma maji 16.

Kazi zingine ni ununuzi wa transfoma na ufungaji njia za umeme wa msongo mkubwa, ununuzi na ulazaji wa mabomba makubwa ya ugawaji maji na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji mitaani yatakayokuwa na urefu wa kilometa 477.
“Maeneo yatakayonufaika na mradi huu ni Salasala, Bunju, Wazo, Makongo, Changanyikeni, Bagamoyo, Mpiji, Zinga, Kiromo, Kitopeni, Ukuni, Kerege, Buma, Mataya na Ukanda maalumu wa EPZA ambayo yanahudumiwa na mtambo wa Ruvu Chini,  Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Msakuzi, Makabe, Malambamawili na Msigani,” anasema Msuya.

No comments:

Post a Comment