Monday, October 30

Rais Magufuli atuma salamu mabadiliko ya CUF


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amepongeza mabadiliko yanayofanywa na Chama Cha Wananchi(CUF) akisema mabadiliko hayo yanaungwa mkono na CCM.
Bila kutaja mabadiliko ya aina gani, Rais Magufuli ambaye alikuwa akizunguza wakati wa ufunguzi wa daraja la furahisha litakalotumiwa na waenda kwa miguu jijini Mwanza amesema,“ tunawapongeza kwa mabadiliko mnayofanya.”
Rais Magufuli amesema hayo wakati akikamilisha hotuba yake na kumtambua Mbunge wa Liwaled, Zuberi Kuchauka(CUF), ambaye awali alipanda jukwaani na kusifia utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Mbunge huyo ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.
Kuchauka ambaye alikaribishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo  Profesa Norman Sigalla King kuwasalimia wananchi mbali ya kumwagia sifa Rais Magufuli pia amesema anamuombea dua ili awe na afya njema kusudi atimize lengo lake na kukuza viwanda na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati.
“Mheshimiwa Rais sisi sote tunatambua kazi nzuri unayoifanya ya kuwaletea maendeleo Watanzania na mimi napenda nikupongeze sana kwa hilo na ndiyo maana nakuombea dua uzidi kuwa na afya njema,” amesema.
Hivyo wakati akikamilisha hotuba yake, Rais Magufuli alimwita Kuchauka jukwaani na kumshukuru kwa namna alivyotambua utendaji wa Serikali yake.
“Yuko wapi yule mbunge wa CUF...njoo hapa. Huyu ni mbunge wa CUF tena ni kaaafu,” alicheka kidogo na kuendelea “hii ndiyo Tanzania ninayoitaka, tofauti za chama siyo uadui. Siyo kila wakati wewe unakuwa wa kupinga tu, kupinga tu huu ni uzito wa mawazo fulani fulani kichwani,” amesema.
Amesema kwa vile mbunge huyo ametoa pongezi kutokana na utendaji mzuri wa Serikali ya CCM basi akamtaka awafikishie salamu wana CUF wenzake kwa yale wanayoendelea kufanya.
“Tunawapongeza sana kwa mabadiliko mnayofanya na ukawafikishie salamu zetu,” amesema Rais Magufuli.
Ingawa Rais Magufuli hakubainisha bayana ni mabadiliko yapi alikuwa akiyazungumzia lakini CUF imekuwa ikikabiliwa na msuguano wa uongozi kiasi kujikuta kikigawika katika pande mbili, ile inayotambulika kama CUF inayoungwa mkono na Maalim Seif na ile nyingine inayojulikana CUF ya Profesa Ibrahim Lipumba.

No comments:

Post a Comment