Jukwaa hilo linatarajiwa kuzinduliwa Oktoba 4 jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo alisema katika taarifa yake kuwa, kuanzishwa kwa jukwaa hilo kunalenga kutatua changamoto mbalimbali zinazotokana na uratibu hafifu wa sekta, taasisi na wadau mbalimbali katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.
Alisema jukwaa hilo litaaInisha kwa kina changamoto zinazoikabili sekta na rasilimali za maji pamoja na kupendekeza utatuzi wake. “Kuzinduliwa kwa jukwaa hili ni fursa ya kubadilishana uzoefu na wadau kutoka sehemu mbalimbali za duniani hususan kuhusu utekelezaji wa mipango ya pamoja ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji,” alisema. “Jukwaa hili pia litatoa mchango wa mambo ya kupewa kipaumbele na Kituo Mahiri cha Rasilimali za Maji kinachotegemewa kuanzishwa hivi karibuni.”
Profesa Mkumbo alisema jukwaa hilo linategemewa kutoa ushauri kwa wizara kuhusu namna bora ya kuboresha ushirikiano baina ya sekta mbalimbali katika usimamizi wa rasilimali za maji.
Kupitia jukwaa wadau wataweza kujifunza, kutoa maoni, ujuzi na kushauri kuhusu masuala mbalimbali ya usimamizi na undelezaji wa rasilimali za maji nchini.
No comments:
Post a Comment