Monday, October 30

Polisi yadhibiti shambulizi la al-Shabab lilouwa 23

Askari akipita karibu na mabaki ya gari lililolipuka mjini Mogadishu, Somalia Jumamosi, Octoba 28, 2017.
Polisi nchini Somalia wamesema Jumapili kuwa wameweza kudhibiti shambulizi la waasi wa kikundi cha Kiislam kilichokuwa  kimeizingira hoteli moja katika mji mkuu Mogadishu.
Maafisa wa polisi wamesema kuwa watu wasiopungua 23 wameuawa katika shambulizi hilo katika hoteli mbili maarufu za Nasa Hablod Mogadishu. Dozeni ya watu wengine walijeruhiwa kutokana na mlipuko huo.
Waasi hao walivamia hoteli Jumamosi, baada ya gari lilokuwa na bomu kulipuka wakati likiwa katika lango la kuingia katika hoteli hiyo.
Polisi wanasema wamefanikiwa kuwakamata washambuliaji wawili na wamewaua wengine wawili.
Kikundi cha waasi wa al-Shabab kimedai kuhusika na shambulizi hilo katika hoteli hiyo.
Kadhalika kulikuwa na mlipuko wa pili Jumamosi karibu na jengo la zamani la bunge. Hata hivyo kiasi cha uharibifu uliotokea katika mlipuko huo hakikuweza kujulikana mara moja.
Milipuko hiyo miwili imetokea wiki mbili baada ya gari kubwa kulipuka na kuuwa watu wasiopungua 358 katika makutano ya barabara mjini Mogadishu kwenye harakati nyingi.
Serikali ya Somalia imekilaumu kikundi cha waasi wa al-Shabab kwa shambulizi lililotokea Octoba, ingawaje kikundi hicho hakijadai kuhusika na shambulizi hilo.

No comments:

Post a Comment