Sunday, October 15

NEC YASISITIZA AMANI NA UTULIVU UCHAGUZI MDOGO WA MADIWANI KATIKA KATA 43

NEC –DODOMA

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Kailima Ramadhan amewaasa wadau wa uchaguzi kuhakikisha kuwa uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika katika Kata 43, Novemba 26 unafanyika kwa amani na utulivu.

Bw. Kailima ameyasema hayo leo (Jumamosi) mjini Dodoma wakati wa maandalizi ya mafunzo kwa Wasimamizi na Wasimamizi wasaidizi pamoja na maafisa uchaguzi yanayotarajiwa kuanza kesho (Jumapili) mjini hapa.

“Mlango wa kuchukua fomu kwa ajili ya uteuzi utafunguliwa kuanzia tarehe 20 saa moja na nusu asuhuhi mpaka 25 mwenzi huu, na fomu zinatakiwa kurejeshwa na uteuzi utafanyika tarehe 26 mwenzi Oktoba saa kumi kamili jioni. Nawasihi wadau wote wa uchaguzi tufanye uchaguzi wetu uwe wa amani na utulivu, natumaini kama ambavyo nchi yetu ni kisiwa cha amani na kwa jinsi tulivyojipanga (Tume) uchaguzi utakua wa amani na utulivu,” amesema.

Bw. Kailima amesema kuwa katika mchakato wa kuendea siku hiyo ya uchaguzi NEC hairuhusu mikutano ya vyama vya siasa bali inaruhusu mikutano ya kampeni.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi hairuhusu mikutano ya vyama vya siasa, Tume inaruhusu mikutano ya kampeni kwa muda wa siku 30 kuanzia tarehe 27 Oktoba mpaka tarehe 25 Novemba 2017, siku moja kabla ya uchaguzi. Kampeni lazima ziendeshwe kwa utaratibu uliopangwa,” amesema Bw. Kailima.

Akizungumzia kuhusu maadili ya Uchaguzi, amesema kwa mujibu wa Kifungu Namba 124A cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Tume, Serikali na vyama vya siasa vyote vinapaswa kukubaliana na maadili ya uchaguzi ambayo yalisainiwa na wadau wote tarehe Julai 27, 2015.

“Nitoe wito kwa wadau wa uchaguzi kwamba pale ambapo patakua na ukiukwaji wa maadili, malalamiko yapelekwe kwenye kamati husika saa 72 baada ya tukio husika, kwa ngazi hii ya udiwani malalamiko yanatakiwa yapelekwe kwenye kamati ya maadili ngazi ya Kata ambayo wajumbe wake ni vyama vyote vya siasa vyenye wawakilishi walioteuliwa. Msimamizi msaidizi ngazi ya Kata ndiyo mwenyekiti wa kamati,” amesema.

Bw. Kailima ameongeza kusema kwamba endapo maamuzi hayataridhiwa wahusika wanaruhusiwa kukata rufaa ngazi ya Jimbo ambapo msimamizi wa uchaguzi atatoa maamuzi na endapo hayakuridhiwa jambo hilo litakua ni lalamiko la uchaguzi baada ya uchaguzi kukamilika.

Mkurugenzi huyo amesema kwamba mafunzo hayo yatahusisha washiriki 144 ambao ni Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimizi wasaidizi na maafisa uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata na yatafanyika kwa siku tatu kuanzia kesho Oktoba 15 hadi 17, 2017.

“Uchaguzi huu mdogo utafanyika kwenye Kata 43 ambazo zipo kwenye mikoa 19, Hamashauri 36 na Majimbo 37 kwa hiyo uchaguzi huu mdogo unafanyika karibia maeneo ya nchi nzima,” alisema Kailima.

No comments:

Post a Comment