Monrovia, Liberia. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Alhamisi iliweka rekodi ya kutangaza rasmi matokeo yote ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 10 ikiwa ni siku sita kabla ya tarehe ya mwisho iliyopangwa Oktoba 25.
Ikitangaza matokeo hayo, NEC imethibitisha kwamba mwanasoka nyota wa zamani duniani, George Weah aliyewania urais kupitia chama cha Congress For Democratic Change (CDC) atachuana na Makamu wa rais Joseph Boakai wa chama tawala cha Unity Party (UP)
Katika uchaguzi huo wa marudio uliopangwa Novemba 7, mshindi ataapishwa kuchukua nafasi ya Rais Ellen Johnson Sirleaf anayemaliza muda wake.
Sirleaf alishinda kwa mara ya kwanza urais mwaka 2006 kuwa rais wa kwanza barani Afrika kuchaguliwa kidemokrasia. Alishinda muhula wa pili mwaka 2011 na atakabidhi madaraka kwa rais wa pili tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipomalizika mwaka 2003.
Matokeo rasmi
Baada ya kujumlisha matokeo yote kutoka vituo 5390 vya kupigia kura vilivyosambaa nchi nzima hakuna mgombea aliyepata asilimia 50+ ya kura za kumwezesha kuwa rais.
Weah alipata kura 596,037 sawa na asilimia 38.4, Boakai kura 446,716 sawa na asilimia 28.8, Cahles Brumskine wa LP kura 149,495 (9.6%), Prince Johnson wa MDR kura 127,666 (8.2%), Alexander Cummings wa ANC kura 112,067 (7.2%) na Benoni Urey wa ALP kura 24,246 (1.6%)
Wagombea wengine 14 waliambulia chini ya asilimia moja ya kura. Wapigakura 1,641,922 sawa na asilimia 75.2 ya waliojiandikisha walishiriki uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment