Sunday, October 29

Mvua kubwa kuendelea kunyesha Tanzania - TMA


Mvua kubwa zanyesha Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani
WAKATI mvua kubwa iliyonyesha jijini Dar es Salaam na mkoani Pwani, Tanzania tayari imesababisha maafa makubwa, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) inasema kuwa mvua kubwa nyingine zinatarajiwa kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa na Magharibi.
Taarifa za TMA zimesema kuwa Mvua kubwa zinatarajiwa Jumamosi na Jumapili katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria na Magharibi ya nchi.
Taarifa ya Mamlaka hiyo iliyotolewa ilisema kuwa vipindi vya mvua kubwa inayozidi milimeta 50 ndani ya saa 24, vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria na Magharibi mwa nchi.
Ilisema kuwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera, Tabora, Katavi na Rukwa itakumbwa na mvua kubwa na kwamba hali hiyo inatokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Tanzania watu watatu walipoteza maisha kutokana na mvua zinazoendelea jijini Dar es Salaam, huku nyumba 100 zikisombwa na maji na nyingine 700 kuendelea kuzingirwa na maji.
Aidha watu wengine wawili walipoteza maisha katika mvua zilizonyesha juzi mkoani Pwani, ambapo miili yao iliopolewa baada ya maji kupungua kwenye Mto Mpiji unaozigawanya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment