Ubomoaji wa nyumba hizo za ibada ni mwendelezo wa uboamoaji wa nyumba takribani 1300 za wakazi wa maeneo hayo zinazodaiwa kujengwa ndani ya mita 121.5 ya barabara hiyo.
Nyumba zaidi ya 1000 zimebomolewa mpaka sasa hali inayosababisha baadhi ya wananchi kulala nje kutokana na kukosa makazi .
Akizungumza na gazeti la Mwananchi leo kwa njia ya simu Mhandisi wa Tanroads Kimara ambaye anasimamia
ubomoaji huo ,Jonson Rutechula amesema kesho watakuwa na kazi maalum ya kubomoa nyumba za ibada tu.
“Tumewaambia viongozi wa misikiti na makanisa, waondoe vitu kesho tunakuja kubomoa.Tutabomoa makanisa 14 na misikiti 10 kuanzia eneo la Kimara hadi Kiluvya”amesema
Amesema shughuli ya ubomoaji wa nyumba imekamilika kwa asilimia kubwa ,zimesalia nyumba za ibada tu.”Kama unavyoona karibu ubomoaji wa nyumba za makazi umekamilika tulibakiza nyumba za ibada”amesema
Ameongeza kwamba “Kesho tutabomoa makanisa 14 na misikiti 10 kuanzia eneo la Kimara hadi Kiluvya na tutaanza kazi hiyo asubuhi”amesema Rutechula.
Hata hivyo mwandishi wetu alitembelea Kanisa la Mtakatifu Maria Parokia ya Kimara na kukuta baadhi ya waumini wakitoa vyombo nje na walipoulizwa baadhi ya viongozi waliokuwepo kanisani hapo walikataa kuzungumza .
“Sisi siyo wasemaji, kama unataka habari njoo kesho na kamera zako uchukue matukio lakini pia mtafute Paroko yeye atakwambia nini kinaendelea maana sisi si wasemaji”amesema mmoja wa waumini hao
No comments:
Post a Comment