Wednesday, October 11

MIAKA 30 KWA WIZI WA SIMU

WAKAZI wanne wa Jiji la Dar es Salaam, wamehukumiwa kwenda jela miaka 30 na kuchapwa viboko 12 kila mmoja kwa wizi wa simu nne za kiganjani.
Watu hao ambao ni wakazi wa eneo la Boko Magengeni katika Wilaya ya Kinondoni, katika kutekeleza adhabu hiyo watachapwa viboko sita wakiingia gerezani na sita siku wakitoka.
Washtakiwa hao walihukumiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage baada ya Jamhuri kuthibitisha makosa yao bila kuacha shaka.
Waliohukumiwa ni Donald Nzwenka,  Michael Paschal, Ally Akili na Kurwa Mwakagenda.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mwijage, alisema washtakiwa kwa pamoja Julai 7, 2013 maeneo ya Boko Magengeni, Dar es Salaam waliiba simu nne aina ya Nokia, Sumsung, Teckno zikiwa na thamani ya Sh 1,300,000.
Pia washatakiwa hao waliiba, fedha taslimu Sh 150,000, cheni za dhababu mbili zenye thamani ya Sh 750,000, ambapo mali yote jumla ina thamani ya Sh 2,050,000.
Hakimu Mwijage alisema kabla ya wizi huo, washtakiwa walimtishia na jambia Hobokela Mwakijambile, ambaye ndiye mwenye mali hizo.
Katika kesi hiyo Jamhuri iliita mashahidi 11 na washtakiwa walijitetea wenyewe.
“Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, mahakama ilijiuliza kwamba kosa la kutumia silaha ili lithibitike Jamhuri wana wajibu wa kuthibitisha bila kuacha shaka kwamba washtakiwa kabla ya kutenda awe na kifaa hatari.
” Pia washtakiwa kabla ya kutenda  wawe zaidi ya mmoja na kwamba baada ya tukio hilo walitumia nguvu kwa mtu aliyeporwa,” alisema.
Alisema katika shauri hilo, mlalamikaji na mashahidi wengine walieleza usiku wa Julai 7 mwaka huo majambazi walivunja mlango mkuu wa nyumba yao kwa kutumia bomu ambalo lilitambuliwa na polisi kuwa baruti.
Ushahidi ulieleza kwamba, washtakiwa waliendelea kuvunja milango mingine na baadae waliingia katika chumba walichokuwa wamekaa mashahidi.
Wakiwa katika chumba hicho chenye mwanga, mshtakiwa wa nne alishika panga na alianza kuwapiga nalo kwa kutumia ubapa.
“Kwa kuzingatia ushahidi huo, hakuna shaka kwamba mashahidi waliweza kuwatambua hao majambazi kwamba ni washtakiwa katika kesi hiyo.
“Kwa kuangalia maelezo yao, waliyotoa Polisi yanaonyesha jinsi walivyoshiriki katika tukio na kwamba washtakiwa ndio walioiba vifaa hivyo kwa kutumia silaha kali,”alisema.
Hakimu alisema utetezi wa washtakiwa kwamba walikamatwa maeneo tofauti na kupelekwa Oysterbay Polisi na kupigwa na kunyanyaswa hauaminiki.
Mahakama ilisema ushahidi huo hauaminiki na hauwezi kupewa uzito wowote. Alisema utetezi wa kukanusha tu kuhusika katika kosa siku hiyo, haukutikisa kwa namna yoyote ushahidi wa Jamhuri.
“Kutokana na hayo, hakuna shaka kwamba washtakiwa walitenda kosa na walitambuliwa ipasavyo.
“Nimeridhika Jamhuri imethibitisha kosa bila kuacha shaka dhidi ya washtakiwa, hivyo nawatia hatiani kwa kosa la kutumia silaha kama walivyoshtakiwa,”alisema.
Jamhuri katika kesi hiyo iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Gloria Mwenda, ambaye alisema washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na akaomba wapewe adhabu kali.

No comments:

Post a Comment