Thursday, October 19

Mazungumzo ya Serikali, Barrick nchi nyingine kujifunza


By George Njogopa, Mwananchi gnjogopa@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema mafanikio yaliyofikiwa baada ya kuwepo majadiliano kati ya wataalamu wa Tanzania na wale wa kampuni ya Barrick Gold Mine kuhusu biashara ya madini ya dhahabu yameweka rekodi ya aina yake hatua ambayo inaweza kuzisukuma nchi nyingine za Afrika kuja Tanzania kujifunza namna inavyoweza kujadiliana na wawekezaji wa kigeni na hatimaye kukubaliana.
“Tanzania tumeonyesha mfano na kweli tukiamua tunaweza. Haya majadiliano hayakuwa kitu rahisi lakini mwisho wa siku tumefanikiwa na naamini nchi nyingine za Afrika zitataka kuja hapa kujifunza namna tulivyofanikiwa,” amesema Magufuli wakati akizungumza leo Alhamisi baada ya kufikiwa makubaliano hayo.
Amesema amejifunza kuwa mazungumzo daima huwa yana faida na licha kuona ugumu wake lakini aliendelea kuiamini timu yake huku akiitia moyo kutorudi nyuma.
Amesema kuanzia sasa Tanzania imeweka kiwango kipya kuhusu mikataba ya madini na kwamba kiwango hicho kilichofikiwa na kampuni ya Barrick ndicho kitatumika katika majadiliano na kampuni nyingine.
“Nasema sasa hili jambo linaendelea pia katika madini mengine ikiwamo Tanzanite na yule asiyetaka basi aondoke atuachie madini yetu... tumepewa na mwenyezi Mungu na tutaendelea kuchukua msimamo huu huu,” amesema.
Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kuwa na moyo wa kizalendo akisisitiza jukumu la kuijenga nchi haitafanywa na raia mwingine wa kigeni bali ni wao.
“Huu ni mwanzo wa kuitengeneza Tanzania yetu na kila Mtanzania lazima ajue wajibu wake maana hakuna mgeni atakayekuja hapa kututengenezea nchi hii,” amesema.

No comments:

Post a Comment