Saturday, October 7

Mapya kwenye mgogoro wa jimbo la Catalonia

Serikali ya Uhispania imesema ushirikiano baina yake na jimbo la Catalonia umevunjika huku serikali hiyo ikiwalaumu viongozi wanaotaka kujitenga kwa jimbo hilo la Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Spanien Barcelona Streik für Unabhängigkeit (Getty Images/AFP/P.-P. Marcou)
Msemaji wa Serikali ya Uhispania  ambaye pia ni waziri wa mambo ya utamaduni, ameitaka  serikali ya jimbo la Catalonia kusitisha juhudi zake za kutaka kujitenga na kuanza majadiliano ya kuutatua mzozo huo. Kwa upande wake kiongozi wa Catalonia Carles Puigdemont anataka kulihutubia bunge la Jimbo wiki ijayo na pia kujadili hali ya kisiasa ya Catalonia licha ya Mahakama ya Katiba ya Uhispania kusimamisha kikao kingine cha wabunge waliotaka kuzungumzia juu ya uwezekano wa kupiga kura ya uhuru wa jimbo hilo.
Katalonien Europa Parlament (Reuters/Reuters TV)
Bunge la Catalonia
Pande zinazovutana nchini Uhispania mapema leo zilionyesha dalili kwamba zinaweza kufanya mazungumzo ya kutafuta njia za kuutatua mgogoro wa kisiasa wa nchini Uhispania baada ya jimbo la Catalonia kupiga kura ya maoni ya kutaka uhuru wake. Serikali ya Uhispania leo kwa mara ya kwanza  imewaomba msamaha  raia wa Catalonia  waliojeruhiwa na polisi wakati wa kupiga kura ya maoni kwa ajili ya uhuru wa jimbo lao, kura ambayo ilipigwa marufuku na seikali kuu.
Waziri mmoja katika serikali ya Catalonia ambaye pia ni mshirika wa karibu wa kiongozi wa jimbo hilo Carles Puigdemont, ameliambia shirika moja la habari kwamba upande wao unaweza kufikiria kusimamisha malumbano katika mgogoro huo, ili kuepuka kuandamwa na serikali kuu ya mjini Madrid.
Katika mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa  kuwahi kutokea nchini Uhispania katika muda wa miongo kadhaa, viongozi wa jimbo la Catalonia walitishia kutangaza uhuru wa jimbo hilo huku waziri mkuu Mariano Rajoy akiapa kuwazuia, na kukataa wito wa kupatanishwa.  Hali hiyo mbaya ya kisiasa inatia hofu ya kulitumbukiza katika machafuko zaid jimbo hilo la kaskazini-mashariki, eneo lenye watu milioni 7.5 na linalopendwa na watalii.  Jimbo la Catalonia linachangia thuluthi moja katika uchumi wa Uhispania.
Ili kuutatua  mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na viongozi wa jimbo la catalonia wanaotaka uhuru wa jimbo hilo, msemaji wa serikali ya Uhispania aliwaambia waandishi wa habari kwamba ni vyema  kuanza kurekebisha mpasuko uliotokea kwa kufanya uchaguzi wa jimbo.
Wakati huo huo Uswisi ambayo haiungi mkono upande wowote imejitolea kufanya mazungumzo baina ya serikali kuu ya Uhispania na jimbo la Catalonia ili kutafuta suluhisho lakini wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imesema muda muafaka wa kufanyika mazungumzo hayo bado haujafika kwa sababu msaada unaweza tu kutolewa iwapo pande zote mbili zitaomba.  Uswisi inasema imewasiliana na pande hizo mbili.  Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uswisi alijibu kwa njia ya baruapepe na kusema mgogoro uliopo nchini Uhispania ni wa masuala ya ndani na hivyo nchi yake inaheshimu uhuru wa Uhispania.

No comments:

Post a Comment