Saturday, October 21

Mapato finyu yaitesa halmashauri ya Siha


Siha. Mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro yameshuka kutokana na uongozi wa halmashauri hiyo kushindwa kuwalipa wenyeviti wa vijiji wanaosimamia ukusanyaji katika maeneo yao
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Frank Tarimo amesema hayo jana Ijumaa katika kikao cha baraza la madiwani.
Amesema miradi mingi katika halmashauri hiyo imekwama kutokana na ukusanyaji wa mapato ya ndani kuwa chini jambo ambalo lisipochukuliwa hatua za haraka litasababisha madhara makubwa.
Tarimo amesema  zaidi ya Sh11milioni zinadaiwa na vijiji kutokana na kufanya kazi ya kukusanya  ushuru wa aina mbalimbali  kwenye miradi  ambayo iko kwenye maeneo yao ikiwemo mageti, masoko pamoja na vituo vya mabasi.
''Wenyeviti wakishirikiana na watendaji tulikubaliana waisaidie halmashauri kukusanya ushuru katika maeneo yao na asilimia 15 watalipwa lakini halmashauri haijafanya hivyo toka Februari mwaka huu hadi sasa,'' amesema Tarimo.
Diwani wa Kata ya Karansi, Dancan Urassa amesema halmashauri kushindwa kulipa asilimia 15 ya makusanyo ya ushuru kwenye maeneo yao imesababisha halmashauri kushindwa kufikia malengo ya makusanyo kwa mwaka huu.
“Hadi sasa halmashauri imefikia asilimia  38 ya ukusanyaji wa mapato ya ndani angali tuna vyanzo vingi sana vya mapato ni vema fedha zinazodaiwa zikatolewa ili kuweza kurudisha ari ya ukusanyaji,” amesema.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Barnabas Mbwambo alikiri kuwepo kwa deni hilo ambapo alifafanua kuwa wameshindwa kutoa asilimia hizo kutokana na kushuka kwa mapato.
Hata hivyo  mkuu wa wilaya hiyo, Onesmo Buswelu amesema malalamiko ya madai ya asilimia 15 za vijiji alipokea na sasa yupo katika hatua za kutatua tatizo hilo ili wenyeviti hao waweze kuendelea na ukusanyaji wao  na kuimarisha hali ya mapato.

No comments:

Post a Comment