Friday, October 13

Makinikia yaendelea kuitesa Acacia


Dar es Salaam. Ikitarajia kuchapisha hesabu zake za fedha kwa robo ya tatu ya mwaka, kampuni ya Acacia inaendelea kuugulia maumivu ya zuio la kutosafirisha mchanga wa madini.
Kwenye taarifa yake ya awali iliyotolewa jana kwa wadau wake na jamii kwa ujumla, kampuni hiyo imeeleza kuimarika kwa uzalishaji lakini ikabainisha kupungua kwa mapato kutokana na zuio hilo lililoanza mapema Machi.
“Mauzo yalikuwa madogo kutokana na zuio la kusafirisha makinikia yanayozalishwa kwenye migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi nchini Tanzania,” inasema taarifa hiyo fupi.
Machi, Serikali ilizuia usafirishaji wa mchanga wa madini na Rais John Magufuli akaunda kamati mbili za kuchunguza uchimbaji, usafirishaji na biashara nzima ya dhahabu ambazo zilibaini udanganyifu unaofanywa hivyo kulinyima Taifa mapato linayostahili.
Licha ya zuio hilo, Serikali ilifanya mabadiliko kwenye sheria za madini ili kuongeza usimamizi wa uzalishaji, udhibiti wa mapato na ushiriki wa Watanzania katika umiliki wa kampuni zenye vibali vya uchimbaji nchini.
Kwa robo nzima ya mwaka, kampuni hiyo inayomilikiwa na Barrick Gold Corporation kwa asilimia 63.9 imezalisha wakia 191,203 na kuuza wakia 132,787. Pamoja na takwimu hizo, changamoto za upatikanaji wa vibali na kupunguzwa kwa uzalishaji kwenye baadhi ya migodi yake kumeathiri kiasi cha dhahabu iliyopatikana.
Vibali viliathiri uzalishaji wa Mgodi wa North Mara ambao umetoa wakia 72,011 ndani ya miezi mitatu ya Julai, Agosti na Septemba wakati Mgodi wa Bulyanhulu ukizalisha wakia 50,094 kutokana na kupunguza operesheni zake.
“Uzalishaji umezidi matarajio katika Mgodi wa Buzwagi uliochangiwa na ubora dhahabu iliyopatikana. Tulizalisha wakia 69,097,” inasomeka taarifa hiyo.
Kuanzia Julai 31, mazungumzo baina ya Serikali na Barrick yanaendelea kutafuta muafaka wa zuio hilo pamoja na kuongeza faida kwa kila upande. Miongoni mwa yanayojadiliwa kwenye mazungumzo hayo ni faini ya Dola 190 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh424 trilioni) ambayo Acacia imeandikiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) ikiwa ni kodi iliyokwepwa pamoja na riba yake.
Tangu kuanza kutekelezwa kwa zuio hilo, bei ya hisa za kampuni hiyo iliyoorodheshwa Soko la Hisa London (LSE) na Dar es Salaam (DSE) imeshuka kutoka Sh12,000 mpaka Sh5,000 kila moja.

No comments:

Post a Comment