Saturday, October 7

Ma-DC wanane akiwamo Mnyeti, RC na DAS washinda uongozi CCM


Dar es Salaam. Wakati Sheria ya Utumishi wa Umma ikuzuia watumishi wa umma kujihusisha na siasa, mkuu wa mkoa, wakuu wanane wa wilaya na katibu tawala mmoja wamejitosa katika chaguzi za CCM na kushinda nafasi za ujumbe wa mkutano mkuu.
Ushindi wao unaibua maswali kuhusu nafasi zao ambazo huanza kuzitumikia baada ya kula kiapo cha kulinda Katiba na cha maadili ya utumishi wa umma.
Viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakilalamikia kuwapo kwa wanachama wa CCM katika nafasi za serikalini na hivyo kufanya upendeleo.
Walioshinda ni mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego ambaye aligombea ujumbe wa mkutano mkuu wa CCM baada ya kupata kura 311.
Mwingine ni katibu tawala wa Wilaya ya Nanyumbu, Salum Palango aliyepata kura 295.
Wakuu wa wilaya walioshinda ni Simon Odunga (Chemba) aliyeshinda kwa kura 432, Christina Mndeme (Dodoma) na Elizabeth Kitundu (Bahi) wote kutoka mkoani Dodoma.
Mkoani Morogoro, walioshinda ni Alhaji Mohamed Utaly (Mvomero) na Seriel Nchembe (Gairo).
Wakuu wengine wa wilaya walioshinda ni Raymond Mushi (Babati) mkoani Manyara, Herman Kapufi (Geita), katibu tarafa wa Makuyuni (Arusha), Paul Kiteleki na mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Alexander Mnyeti.
Mnyeti ambaye katika siku za karibuni, ameingia katika tuhuma za kutumia ofisi kushawishi madiwani wajiunge na CCM ambazo zilitolewa kwa picha za video na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, alishinda baada ya kupata kura 266 akiwa hayupo ukumbini.
Katika nafasi hiyo ambayo ilikuwa inagombewa na wanaCCM 22, wajumbe wengine waliochaguliwa ni mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Elishilia Kaaya aliyepata kura 258 na Dk Daniel Mirisho aliyepata kura 327.
Uchaguzi huo uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Makumira ulisimamiwa na mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake ya Arusha, Mary Kisaka.
Waraka mkuu Namba 1, 2000 wa Maadili ya Watumishi wa Umma unazuia watumishi hao kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika chama, lakini hauwataji wakuu wa mikoa wala wa wilaya.

No comments:

Post a Comment