Lundu anayemtetea mshitakiwa wa nne, Jalila Zuberi, wa sita, Sadick Mohamed na wa saba Ally Mussa Majeshi, ndiye aliyekuwa amuhoji shahidi wa kwanza wa mashitaka, Koplo Seleman Faraji.
Mawakili wenzake, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu na Emanuel Safari walishamaliza kumuhoji shahidi huyo katika kesi ndogo Ijumaa Oktoba 27,2017 na leo Jumatatu Oktoba 30,2017 alikuwa amalizie Lundu.
Hata hivyo, baada ya Mahakama kuanza, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula alimjulisha Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo kuwa Lundu amepata dharura.
Chavula ameiomba Mahakama iahirishe kesi hiyo hadi kesho Jumanne Oktoba 31,2017, ombi lililoungwa mkono na wakili Safari kwa niaba ya mawakili wenzake wa utetezi na Jaji Maghimbi ameliridhia.
Kesi hiyo ndogo iliibuka baada ya mawakili wa utetezi kupinga kupokewa maelezo ya kukiri kosa ya mshitakiwa wa pili, Shaibu Jumanne wakidai aliyatoa baada ya kuteswa na polisi.
Koplo Seleman ameieleza Mahakama kuwa Agosti 16,2013 baada ya kumkamata mshtakiwa eneo la Mirerani wilayani Simanjiro alipewa jukumu la kuandika maelezo yake katika Kituo cha Polisi Mirerani.
Katika maelezo hayo ambayo alidai aliyatoa kwa hiari na bila kulazimishwa, mshitakiwa alikiri kushiriki tukio la kumuua mfanyabiashara huyo.
Hata hivyo, shahidi huyo alipoiomba Mahakama ipokee maelezo hayo kama kielelezo cha kesi hiyo, jopo la mawakili wa utetezi likiongozwa na Majura Magafu lilipinga na kutoa sababu nne.
Magafu alisema mshitakiwa amemweleza kuwa hakuandika maelezo polisi Agosti 16,2013 kwa kuwa siku hiyo hakuwa amekamatwa na polisi.
Pia, alisema anachojua ni kuwa Agosti 18,2013 ndipo alipoteswa na polisi na kulazimishwa kusaini maelezo ambayo hakuyatambua.
Wakili Magafu alisema maelezo aliyolazimishwa mteja wake kusaini na kuweka dole gumba hakuwahi kusomewa wala kujua kilichoandikwa na hajui chochote kuhusu tukio hilo.
Magafu alisema baada ya mshitakiwa kuteswa na kuumizwa, polisi waliingiwa woga angeweza kufia Kituo cha Polisi Moshi hivyo Agosti 21,2013 walimpeleka hospitali.
Amesema mshitakiwa alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi na baadaye kuendelea kutibiwa katika zahanati ya Gereza la Karanga hadi alipozidiwa akapelekwa KCMC.
Baada ya kutoa hoja hiyo, wakili Chavula alisema msimamo wa kisheria linapojitokeza suala la iwapo mshitakiwa alitoa maelezo kwa hiari au la, ni lazima kuwe na kesi ndani ya kesi.
Akitoa ushahidi katika kesi ndogo, Koplo Seleman alisisitiza kuwa wakati akichukua maelezo ya mshtakiwa alikuwa na afya njema na hakuwa na jeraha lolote. Kesi itaendelea kesho Jumanne Oktoba 31,2017
No comments:
Post a Comment